Kesho ni Siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, na wakati Watanzania wakiingia vituoni kupiga kura, wito maalum wa kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa unatolewa na viongozi wa dini nchini.
Katika Kongamano la Viongozi wa Dini Kanda ya Kati, lililofanyika jijini Dodoma siku mbili zilizopita, viongozi hao walisisitiza umuhimu wa wananchi, hasa vijana, kutambua nafasi yao kama nguzo ya Taifa na kutumia siku ya leo kwa hekima, uwajibikaji na uzalendo.
Akizungumza katika kongamano hilo, Askofu Evance Chande, wa Kanisa la Carmel Assemblies of God, aliwakumbusha Watanzania kuwa vijana ndio nguvu ya Taifa, hivyo wana jukumu la kulinda amani na kutumia kura kama silaha ya maendeleo. Askofu Chande alisisitiza: “Tunapaswa kuikumbatia amani kama tunavyokumbatia imani zetu. Uchaguzi ukipita, Tanzania inabaki kuwa moja. Tusikubali kugawanywa kwa misingi ya kisiasa.”
Kaulimbiu ya kongamano hilo ilikuwa, "Kupiga kura ni haki ya kila Mtanzania, amani na utulivu ni jukumu letu." Sheikh Mustapha Rajab, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, aliyekuwa mgeni rasmi, aliungana na wito huo, akisema: “Amani si jambo la bahati mbaya, ni matokeo ya utii, uvumilivu na kuheshimu mamlaka. Tukitii viongozi wetu wa dini na Serikali, Taifa litaendelea kubaki salama.”
Wito wa jumla kwa wananchi ni kuendelea kuliombea Taifa, kuonyesha uvumilivu na maelewano, huku wakisisitiza kwamba amani ni msingi wa maendeleo, imani, na utajiri mkubwa zaidi wa Tanzania.
Wakati huo huo, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imethibitisha utayari wake kamili wa kusimamia uchaguzi wa kesho. Mwenyekiti wa INEC, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele, alitoa risala ya namna ya kufanikisha uchaguzi na akiwa Mkoa wa Katavi kujionea maandalizi ya ujenzi wa vituo 83 vya kupigia kura vilivyotengwa maalum kwa ajili ya wakazi wa maeneo yaliyofutwa kiutawala, INEC iko tayari kwa uchaguzi.
Jaji Mwambegele alisema Tume imetoa matangazo katika maeneo yote yaliyofutwa na imeweka vituo katika maeneo jirani ili kuwawezesha wapiga kura kushiriki. Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Tanganyika, Bi. Kagemlo Mutagwaba, alihakikishia kuwa wapiga kura kutoka maeneo hayo wamehamasishwa na wanaonyesha utayari wa kujitokeza kupiga kura kesho.
Post a Comment