TAARIFA KWA UMMA
Kesho, Oktoba 29, 2025, Tanzania inaingia kwenye historia nyingine muhimu kwa kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Taifa.
Katika kipindi hiki cha kihistoria, tunaliomba Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi na usalama kwa waandishi wa habari watakaokuwa wakitimiza majukumu yao ya kitaaluma katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Wakati wananchi wengine watapiga kura na kurejea nyumbani, waandishi wa habari watakuwa kazini kwa muda wote kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi, kwa wakati na bila upendeleo. Hivyo basi, usalama wao ni wa msingi.
Jeshi la Polisi lina dhamana ya kulinda raia na mali zao. Ni muhimu kutambua kuwa waandishi wa habari ni sehemu muhimu ya mchakato wa uchaguzi, na uwepo wao katika vituo vya kupigia kura na maeneo mengine ya uchaguzi ni wa kiutumishi kwa Taifa.
Pamoja na wito huo, nawakumbusha waandishi wa habari wote kufanya kazi zao kwa weledi, uwajibikaji na kuzingatia maadili ya taaluma ili kuepuka migongano ya kimaslahi au migogoro isiyo ya lazima.
Ikumbukwe kuwa, usalama wa mwandishi wa habari unaanza na yeye mwenyewe.
Natoa pia rai kwa waandishi wa habari wote kutambua kuwa wana jukumu kubwa la kulinda amani, umoja na mshikamano wa Taifa la Tanzania wakati huu muhimu wa uchaguzi.
Aidha, waandishi wote wanakumbushwa kuvaa “press jackets” zao kwa utambulisho na usalama wao, isipokuwa pale tu itakapokuwa ni muhimu kutovaa kwa sababu za kiusalama zaidi.
Mwisho, nawakumbusha waandishi wa habari wote kutumia haki yao ya kimsingi ya kupiga kura kama raia wengine wa Tanzania, sambamba na jukumu lao muhimu la kuihabarisha jamii.
Imetolewa na:
Edwin Soko
Mwandishi wa Habari Mwandamizi
Mtetezi wa Haki za Binadamu

Post a Comment