"
VIJANA KAHAMA WAKATAA MAANDAMANO, WAAPA KULINDA AMANI
Na Mwandishi wetu - KahamaVijana wilayani Kahama mkoani Shinyanga wamewaomba vijana wenzao nchini kuungana kwa pamoja kuilinda na kuienzi amani iliyopo kama tunu muhimu kutoka kwa waasisi wa Taifa la Tanzania.Vijana hao kutoka katika kada mbalimbali ikiwemo walinzi wa jeshi la jadi (sungusungu), machinga, mama lishe, maafisa usafirishaji (bodaboda, bajaji) pamoja na wachimbaji wadogo, wamesema hawako tayari kutumika kuvuruga amani ya nchi, badala yake wataungana kuiilinda ili waweze kufanya shughuli zao kwa uhuru na kutimiza malengo yao.Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, mbele ya mkuu wa wilaya hiyo Frank Nkinda, wakati wa kongamano lililoandaliwa na vijana wa Kahama, jana Oktoba 27, 2025, katika viwanja vya magereza Kahama, wamesema hawaungi mkono vitendo vyovyote vinavyoashiria uvunjifu wa amani wilayani humo.Vijana hao akiwemo William Mondi msemaji wa jeshi la jadi (sungusungu) Kahama amesema, “Sisi kama wapenda amani tunapenda amani iliyopo iendelee, sisi sote vijana wa Kahama na Tanzania niwaombe tuienzi amani tuliyoachiwa ndio tunu pekee na alama ya Taifa letu duniani.”Nae mwenyekiti wa umoja wa machinga wilaya ya Kahama Idrisa Kayombo amesema amani iliyopo nchini imewawezesha kufanya biashara zao bila usumbufu ikiwemo kusafirisha mizigo yao kutoka ndani na nje ya nchi. “Amani iliyopo imelindwa karne na karne, mpaka sasa sisi tunanufaika nayo, sisi machinga tunasafiri usiku na mchanga ndani na nje ya nchi na kusafirisha bidhaa zetu, tunasomesha, tunafanya maendeleo, ni kwa sababu ya amani hii, tunaahidi hatutaivuruga.”AmesemaNa kuongeza “Tunaona kwenye mitandao eti Oktoba 29, tuandamane tusipige kura, sisi machinga Kahama hatutaandamana, tutapiga kura, tutaenda kufanya biashara zetu, tutimize mahitaji ya familia zetu na wanaotutegemea.”Katibu wa wajasiriamali wilaya ya Kahama Devetha Henry amesema, “Kwa niaba ya wajasiriamali kundi la wanawake hapa Kahama hatupo tayari kuichezea amani yetu, hatutaandamana Oktoba 29, kwa sababu ikitokea machafuko, wa kwanza kuathirika ni wanawake na watoto wetu, wanawake wenzangu tukapige kura tuache ushabiki tutapoteza watoto wetu.”Kwa upande wake mwenyekiti wa maafisa usafirishaji wa pikipiki za magurudumu mawili na matatu mkoa wa Shinyanga, Idisam Mapande amesema, msimamo wa maafisa usafirishaji Kahama ni kupiga kura na kubeba abiria na si vinginevyo.Amesema “Kahama ni lango kuu la kibiashara katika nchi yetu, watu wote wanaotoka nchi za magharibi kuingia Tanzania mji mkubwa wa kwanza wa kibiashara ni Kahama, kwa hiyo kinachofanyika huenda wanaimezea mate Kahama yetu inavyonawirika, wanataka kutuharibia mkate wetu, hatutakubali.”Na kuongeza “Wanaohamasisha maandamano tunayoyaona kwa njia ya mtandao wapo nchi za nje na familia zao, sisi hatutashiriki hayo maandamano badala yake tutashiriki uchaguzi, na kisha tukapige buku buku zetu kwa abiria.” Tito Okuku ni mzee mwenye miaka 72, amewasihi vijana kutokukubali kutumika kuvuruga amani ya nchi, na kwamba amai iliyopo ndiyo iliyomuwezesha kufikia umri alionao.“Mimi nina umri wa miaka 72 sasa hivi, nimefika hapa kwa sababu ya amani iliyopo Tanzania, tungependa nyinyi vijana muendelee kuwa na amani iliyotulea sisi, vijana wanashawishika haraka sana, na mlipoona kuna mambo hayapo sawa mkaalika hili kongamano, mimi niwaambie, ‘msitumike’.” Amesema mzee OkukuKwa upande wake mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda amewapongeza vijana wa Kahama kwa hatua hiyo kubwa na kuwahakikishia kuwa usalama umeimarishwa vya kutosha na kila mmoja ajitokeze kupiga kura.Amesema “Vyombo vyote vya ulinzi na usalama vipo imara, Kahama ni salama sana, ninawapongeza na kuwashukuru sana vijana kwa ushirikiano, na yeyote atakaeonyesha dalili za uvunjifu wa amani nipeni taarifa.”Amesema “Sikutegemea kama vijana wenzangu mngefanya jambo hili kubwa, mimi niwapongeze kwa niaba ya serikali, niwahakikishie ushirikiano usiku na mchana, wafikishieni salamu, Kahama si sehemu salama kwa mtu ambaye anadhani atajikuna akiwa barabarani na kuwaathiri wananchi wanajitokeza kupiga kura.”Mwisho.
Mkuu wa wilaya ya Kahama Frank Nkinda, akizungumza wakati wa kongamano lililoandaliwa na vijana wa Kahama.





Post a Comment