Na. Belnardo Costantine, Misalaba Media
Maafisa wa Idara ya Uhamiaji Tanzania zaidi ya 20 wamefanya ziara ya kimafunzo katika Jamhuri ya Watu wa China ili kuwajengea uwezo.
Ziara hiyo imeandaliwa kwa pamoja kati ya Serikali ya Jamhuri ya watu wa China na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Xi Ping wa Jamhuri ya Watu wa China na ilianza tarehe 15 Oktoba, 2025 huku ikitarajiwa kuhitimishwa tarehe 31Oktoba 2025.
Akizungungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi Msaidizi wa Uhamiaji -Guanghzou Zhao Huiame ambaye ndie mwenyeji wa mafunzo hayo alisema Jamhuri ya watu wa China inathamini na kutekeleza kwa vitendo katika kuendeleza ushirikiano wa kihistoria baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China na kwamba ni jukumu lao kuhakikisha Mataifa rafiki pamoja na Tanzania yako mstari wa mbele katika kupambana na uhalifu unaovuka mipaka.
Kwa upande wake kiongozi wa timu ya Maafisa uhamiaji hao SSI Richard Mwasongwe aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwapa nafasi pia alimshukuru Kamishna Jenerali wa Uhamiaji CGI Dkt. Anna Makakala kwa Jitihada zake za kuhakikisha kuwa maafisa wanaendelea kupata nafasi ya kujifunza nje ya Nchi Kwa Manufaa ya Idara na Taifa Kwa ujumla.
Mafunzo hayo yalilenga kujifunza kwa nadharia na vitendo ambapo Maafisa hao Waandamizi walifanikiwa kutembelea Uwanja wa ndege wa Baiyun (Baiyun Internationa Airport) na kituo maalum cha Uhamiaji cha Bandari ya Nansha (Nansha Port) katika mji wa Shenzen ambayo kwa kiasi kikubwa inatumia akili mnemba kujiendesha.
Ziara hiyo ya mafunzo pia iliwapa maafisa hao fursa ya kutembelea Kituo jumuishi cha huduma za uhamiaji (OSBP) kilichopo katika mji wa Hongkong ambao umeunganishwa na daraja linalopita baharini kwa zaidi ya kilomita 55 (Hong Kong- Zhuhai- Macao bridge), ambapo walijionea huduma za Uhamiaji zinavyofanyika katika kituo hicho jumuishi chenye mfumo wa e-gate.



Post a Comment