" MAHAFALI YA MULEBA LUTHERAN VTC YANG'ARA; MKUU WA CHUO AJIVUNIA MAFANIKIO NDANI YA MIEZI MITATU.

MAHAFALI YA MULEBA LUTHERAN VTC YANG'ARA; MKUU WA CHUO AJIVUNIA MAFANIKIO NDANI YA MIEZI MITATU.


Na Lydia Lugakila, Misalaba Media MULEBAMahafali ya Chuo cha Muleba Lutheran (VTC) yamefana kwa kiwango kikubwa, huku mkuu wa chuo hicho, Jaspa Elias Masilingi, akieleza kujivunia mafanikio makubwa yaliyopatikana ndani ya kipindi kifupi cha miezi mitatu tangu achukue uongozi.Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Masilingi amesema amefurahishwa na ushirikiano alioupata kutoka kwa wazazi, walimu na wanafunzi, jambo alilolieleza kuwa limempa hamasa ya kuendelea kuinua kiwango cha elimu na nidhamu katika taasisi hiyo.Amebainisha kuwa chuo hicho kimesajiliwa chini ya Wizara ya Elimu kwa ajili ya kutoa mafunzo stadi, na jumla ya wanafunzi 17 wamehitimu baada ya kusoma kwa miaka miwili katika fani za Tehama na Umeme wa Majumbani.Baadhi ya wahitimu, akiwemo Ashrafu Sadu na Malina Alistides, wamesema elimu na ujuzi walioupata chuoni hapo umeandaa uwezo wao wa kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii. Wameeleza kuwa, mbali na masomo ya kitaaluma, wamepata pia elimu ya kilimo ikiwemo uzalishaji wa mbogamboga, matunda na ndizi—maarifa ambayo yanaongeza fursa zao za kujiajiri.Kwa upande wao, wazazi wa wahitimu wameushukuru uongozi wa chuo kwa kutoa elimu ya ujuzi inayokidhi mahitaji ya soko la ajira katika mazingira ya sasa ya kiuchumi.Naye Mgeni rasmi, Luther Lutashobya kutoka ELCT Bukoba, amewahimiza wahitimu wa Tehama kutumia vyema fursa za ukuaji wa teknolojia, akisisitiza kuwa dunia ya sasa inategemea matumizi ya mtandao hivyo ujuzi wao una umuhimu mkubwa. Aidha amewasihi wahitimu kuendelea kujifunza, kuwa waaminifu na kuzingatia maadili ili kujijengea sifa na kuaminika katika maeneo wanayokwenda kufanya kazi. Lutashobya ,ametoa wito kwa wafanyajazi kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na moyo wa kujitoa kwa manufaa ya jamii.


Post a Comment

Previous Post Next Post