" SHIRIKI LA UMEME MKOA WA RUVUMA WAWATAKA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA ULINZI NA UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU YA USAFIRISHAJI UMEME

SHIRIKI LA UMEME MKOA WA RUVUMA WAWATAKA WANANCHI KUSHIRIKI KATIKA ULINZI NA UTUNZAJI WA MIUNDOMBINU YA USAFIRISHAJI UMEME

Maafisa wa Shirika la Umeme Mkoa wa Ruvuma wamekutana na wananchi wa Kijiji cha Madinga katika Halmashauri ya Madaba kupitia mkutano maalum wenye lengo la kutoa elimu kuhusu umuhimu wa kulinda na kutunza miundombinu ya umeme inayopita katika maeneo yao. Mkutano huo umefanyika baada ya kubainika kwamba maeneo mengi yanayopitiwa na njia za kusafirisha umeme hukabiliwa na changamoto ya uvunjifu wa taratibu za usalama na uharibifu wa miundombinu.Akizungumza katika mkutano huo, Injinia Masule Masaga, Mhandisi wa Usafirishaji Umeme Mkoa wa Ruvuma na Njombe, alisema kuwa suala la kulinda miundombinu ni la kila mwananchi, kwani usalama wa umeme unaathiri maisha na shughuli za kiuchumi za jamii nzima. Alibainisha kuwa Kijiji cha Madinga ni miongoni mwa vijiji 50 vilivyopitiwa na mradi mkubwa wa kusafirisha umeme, hivyo wameingia makubaliano ya ulinzi wa miundombinu hiyo pamoja na serikali ya kijiji ili kuhakikisha hakuna shughuli za kibinadamu zitakazohatarisha miundombinu hiyo.Kwa upande wake, Injinia Liberatus Juma, Msimamizi wa Njia za Usafirishaji Umeme Mkoa wa Ruvuma na Njombe, alieleza kuwa laini ya umeme iliyopita katika kijiji hicho ni ya kiwango cha kitaifa (National Grid) yenye uwezo wa kilovoti 220, sawa na volt 220,000, ambayo ni zaidi ya mara 1000 ya umeme wa majumbani. Alisema kiwango hicho kikubwa cha umeme kinahitaji usimamizi makini na utii wa sheria za usalama ili kuepusha madhara kwa watu na mali.Aidha, alisisitiza kuwa maeneo yote yanayopitiwa na njia ya kusafirisha umeme hutengwa rasmi na wananchi hulipwa fidia ili kuhakikisha hakuna shughuli nyingine za kibinadamu zitakazofanyika chini ya laini hizo. Aliwataka wananchi waendelee kuwa walinzi wa miundombinu hiyo kwa kutoa taarifa pindi wanapoona vitendo vya uharibifu, kwani usalama wa miundombinu ya umeme ni msingi wa maendeleo na upatikanaji wa huduma bora za umeme nchini.

 


Post a Comment

Previous Post Next Post