Na, Egidia Vedasto,
Misalaba Media, Arusha.
Mkuu wa mkoa Arusha CPA Amos Makalla ameahidi kufanyia kazi changamoto mbalimbali wanazopitia waendesha bodaboda (Maafisa usafirishaji) Jijini Arusha.
Amesema hayo katika mkutano uliowakutanisha waendesha bodaboda na bajaji ambapo amesikiliza kero zao na kuwaahidi kuzifanyia kazi sambamba na kuwapeleka nchini Rwanda wapate maarifa ya namna bora ya kufanya kazi zao.
Aidha amesisitiza suala la kauli nzuri kutoka kwa watumishi kuwapa nafasi wananchi kutoa maoni na kueleza changamoto zao badala ya kuwakatisha tamaa na kupuuza changamoto zao.
"Nawasihi itunzeni ahadi ya kuendelea kushirikiana na serikali kwa kuendelea kusaidia wananchi wanaotumia vyombo vyenu vya usafiri, wanaovitumia hadi usiku wa manane wakiwemo mama ntilie, wagonjwa na wengineo",
"Mniombee niendelee kuwepo katika mkoa huu ili nitimize maono yangu juu yenu" amesema.
Hata hivyo amesisitiza kuwa waendesha bodaboda (Afisa usafirishaji) waheshimiwe kwa kazi yao maana ni kazi kama kazi nyingine na ni wasomi.
Mmoja wa waendesha bodaboda Kata ya Kimandolu Godlisten Evarest amemuomba mkuu wa mkoa kuwasidia kupata viongozi wapya akiwemo mwenyekiti kufuatia mwenyekiti aliyekuwepo kupoteza maisha katika machafuko ya Oktoba 29.
"Nakuomba utusaidie kupata viongozi wapya maana hata waliobaki wanakula pesa zetu hawana msaada, tukihoji hawatoi majibu ya kueleweka, vile vile naomba Polisi waache kukamatakamata watu kwa kuangalia sura bali wazingatie makosa" amesema Godlisten.
Vilevile Vedasto Msukuma afisa usafirishaji kata ya Ungalimited ameomba waendesha bodaboda na bajaji wote kuwa na vitambulisho vitakavyowatambulisha kwa wateja wao.
"Mimi Rwanda nimeenda, Uganda nimefika lakini waendesha bodaboda wa huko wanaonyesha kuvutia na ustarabu wa kazi kwa sababu kuna utaratibu wa vitambulisho. Wanaonekana wako smati kuliko sisi kwa sababu hiyo" amesisitiza Msukuma.
Akifunga kikao hicho CPA Makalla alimuagiza mkuu wa Wilaya ya Arusha Joseph Mkude aliyekuwa ameongozana nae kutatua mgogoro wa uongozi wa bodaboda ndani ya siku saba na kumpatia taarifa.
Amesema kero zingine ikiwemo Barabara atazifuatilia na kuzipatia majibu haraka na kumuagiza mkurugenzi wa Jiji la Arusha kutoa elimu ya namna ya bodaboda wanaweza kupewa mikopo na masharti wanayopaswa kuwa nayo.
Amesema alichogubdua katika kikao hicho ni kukosekana Kwa taarifa sahihi ya namna mikopo inavyotolewa lakini si kweli kwamba mikopo haitolewi.
Awali kaimu mkurugenzi wa Jiji la Arusha, na Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Shaban Manyama alisema Jiji limekuwa likitoa mikopo Kwa vikundi vya vijana, wanawake na walemavu na bodaboda ni miongoni mwa wanufaikaji ambao zaidi ya milioni400 wameweza kukopeshwa.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment