Na Mwandishi Wetu, Handeni TC
Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Salum Nyamwese, amesema wilaya hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha wananchi wanahamasika kujiunga na Bima ya Afya kwa Wote ili kuwa na uhakika wa kupata huduma bora za matibabu.
Akizungumza mjini Handeni, Mhe. Nyamwese amesema kuwa katika wilaya hiyo yenye Halmashauri ya Mji Handeni na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miundombinu ya kisasa ya kutolea huduma za afya.
Amesema kuwa katika kuhakikisha wananchi wananufaika na bima ya afya kwa wote, wilaya imejiandaa kikamilifu kwa kuweka mazingira wezeshi ya utoaji huduma ikiwemo upatikanaji wa vituo vya afya, vifaa tiba, dawa pamoja na rasilimali watu.
“Wilaya yetu tumejipanga na tuna mikakati madhubuti ya kuhakikisha tunamsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kutimiza ahadi yake kwa Watanzania ya kuhakikisha wanapata huduma bora za afya kupitia bima ya afya kwa wote,” amesema Mhe. Nyamwese.
Amebainisha kuwa ndani ya wilaya ya Handeni kuna jumla ya vituo 84 vya kutolea huduma za afya ambavyo vimepatiwa vifaa tiba kulingana na ngazi ya utoaji huduma.
Aidha amesema huduma za kibingwa zinatolewa katika hospitali za wilaya kwa kushirikiana na wataalamu kutoka hospitali za rufaa za kikanda, hatua inayolenga kuhakikisha wananchi wanapata huduma karibu na maeneo yao.
Kuhusu upatikanaji wa dawa, Mkuu wa Wilaya amesema kuwa kwa sasa hali ni nzuri kwani zaidi ya asilimia 90 ya dawa zinapatikana katika hospitali zote za wilaya.
Ameongeza kuwa wilaya inatarajia kupokea wataalamu zaidi wa afya ili kuimarisha utoaji wa huduma, kutokana na Serikali tayari kuwekeza katika miundombinu na vitendea kazi.
“Nitoe wito kwa wananchi kutumia fursa ya bima ya afya kwa wote. Tusiiache itupite. Tutatangaziwa utaratibu wa kujiunga nayo na ni muhimu sisi wananchi kuwa mstari wa mbele kunufaika na fursa hii, kwani ina faida kubwa katika kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za afya,” amesisitiza Mhe. Nyamwese.

Post a Comment