" JESHI LA POLISI LATHIBITISHA HALI YA USALAMA NCHINI SHWARI YATOA ANGALIZO KUELEKEA SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA

JESHI LA POLISI LATHIBITISHA HALI YA USALAMA NCHINI SHWARI YATOA ANGALIZO KUELEKEA SIKUKUU ZA MWISHO WA MWAKA

 

Jeshi la Polisi Tanzania limetoa taarifa kwa umma likiwahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama nchini imendelea kuwa shwari katika kipindi cha siku 10 tangu kutolewa kwa taarifa ya awali mnamo tarehe 12 Desemba 2025.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa leo tarehe 22 Desemba 2025 kutoka Makao Makuu ya Polisi Dodoma, imeelezwa kuwa licha ya utulivu huo, kumeripotiwa matukio machache ambayo tayari yameshughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi na mikataba ya kimataifa.

Ulinzi Wakati wa Sikukuu Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa linaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi nchini wakati huu wa kuelekea sherehe za Krismas na Mwaka Mpya. Lengo ni kuhakikisha usalama unakuwepo wakati wote wa sikukuu na hata baada ya hapo ili wananchi waweze kushiriki katika ibada, shughuli za kijamii, na kutumia muda na familia zao bila bughudha.

Wito kwa Wananchi Jeshi la Polisi limetoa wito kwa Watanzania na wageni wote waliopo nchini:

Kulinda Amani: Kila mmoja kutambua thamani ya amani na utulivu kama nyenzo kuu ya kuwezesha ufanyaji wa shughuli halali za kila siku.

Kukataa Vurugu: Wananchi wameaswa kukataa mipango yoyote inayolenga kuvuruga amani katika kipindi hiki cha sikukuu na baada ya hapo.

Usalama Barabarani: Kwa wale wanaosafiri, Jeshi la Polisi limewataka kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali, likikumbusha kauli mbiu ya: "Endesha Salama, Familia inakusubiri".

Taarifa hiyo imehitimishwa kwa kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa pamoja kati ya wananchi na vyombo vya dola ili kuendelea kuimarisha amani nchini.

Post a Comment

Previous Post Next Post