
Tumaini jipya la kuendelea kuishi limeanza kuchomoza kwa Jenipha Paskali (28), mkazi wa Kata ya Olasiti Jijini Arusha, baada ya mama yake kuonesha utayari wa kumtolea figo moja ili kuokoa maisha ya binti yake anayesumbuliwa na tatizo la kushindwa kwa figo kufanya kazi.
Kwa mujibu wa simulizi ya Jenipha, afya yake ilianza kudorora baada ya muda mrefu wa kutokunywa maji ya kutosha, hali aliyodai ilichangia figo zake kushindwa kufanya kazi ipasavyo. Tangu kugundulika kwa tatizo hilo, maisha yake yamebadilika kwa kiasi kikubwa, yakigubikwa na maumivu, hofu na gharama kubwa za matibabu ya mara kwa mara.
Akizungumza na waandishi wa habari akiwa katika chumba alichopanga Olasiti, Jenipha alisema kuwa tangu Aprili mwaka huu amekuwa akitumia fedha nyingi kwa ajili ya matibabu, ikiwemo huduma ya kusafisha figo (dialysis). Alifafanua kuwa hadi sasa tayari ametumia zaidi ya shilingi milioni 20 akijaribu kupambana na hali hiyo ili kuendelea kuishi.
“Ni hali ngumu sana. Kila wiki natakiwa kufika hospitali kwa ajili ya kusafisha figo, na gharama zake ni shilingi laki sita kwa wiki. Si rahisi, hasa kwa mtu asiye na kipato cha uhakika,” alisema Jenipha kwa masikitiko, akiongeza kuwa gharama hizo zimekuwa mzigo mkubwa kwake na kwa familia yake.
Katika hatua ya kuokoa maisha yake, madaktari wamemshauri afanyiwe upasuaji wa kuhamishiwa figo (kidney transplant). Hata hivyo, gharama za zoezi hilo ni kubwa zaidi. Jenipha alisema kuwa jumla ya shilingi milioni 45 zinahitajika ili kufanikisha upasuaji wa kuhamishiwa figo ya mama yake, ambaye amekubali kwa hiari kuchangia figo moja kwa ajili ya binti yake.
“Mama yangu ameonesha moyo wa kipekee. Ameamua kunisaidia bila kusita, licha ya hatari na changamoto zinazoweza kujitokeza. Yeye ndiye tumaini langu kubwa lililobaki,” alisema Jenipha huku akishindwa kuficha hisia zake.
Kwa upande wake, familia ya Jenipha imeeleza wasiwasi wao kuhusu uhitaji wa fedha hizo kwa haraka, ikisema kuwa bila msaada wa wadau, ndoto ya upasuaji huo inaweza kuwa ngumu kutimia. Wamewahimiza watu wenye uwezo, taasisi na mashirika ya kijamii kujitokeza kusaidia ili kuokoa maisha ya binti yao.
Wataalamu wa afya wameendelea kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kunywa maji ya kutosha na kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, wakisisitiza kuwa matatizo ya figo yanaweza kuzuilika endapo tahadhari zitachukuliwa mapema.
Kwa Jenipha, upasuaji wa kuhamishiwa figo unamaanisha mwanzo mpya wa maisha, kuondokana na gharama za kila wiki za dialysis, na kurejea katika shughuli za kawaida. Anasema anaamini kwa msaada wa jamii na moyo wa kujitoa wa mama yake, bado ana nafasi ya kushinda vita hii ya uhai.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment