" MCHUMI NA MCHAMBUZI WA SIASA EVANCE KAMENGE AWATAKIA WAKRISTO NA WATANZANIA HERI YA KRISMASI NA MWAKA MPYA 2026

MCHUMI NA MCHAMBUZI WA SIASA EVANCE KAMENGE AWATAKIA WAKRISTO NA WATANZANIA HERI YA KRISMASI NA MWAKA MPYA 2026


Na Lydia Lugakila, Misalaba Media

Kagera

Mchumi na mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka mkoani Kagera, Evance Kamenge, amewatakia Wakristo pamoja na Watanzania wote kwa ujumla heri ya Sikukuu ya Krismas na Mwaka Mpya 2026 huku akiwataka kusherehekea sikukuu hizo kwa amani, upendo na mshikamano.

Akizungumza katika ujumbe wake wa sikukuu, Kamenge amesema Krismasi ni kipindi muhimu cha kutafakari upya maisha, kuimarisha mahusiano ya kijamii na kujenga taifa lenye misingi ya haki, umoja na maendeleo.

“Krismasi ni wakati wa kuimarisha upendo, kusameheana na kudumisha amani. 

Niwaombe Watanzania wote tusherehekee sikukuu hizi kwa furaha, mshikamano na kuheshimiana, tukitanguliza maslahi ya taifa letu,” amesema Kamenge.

Kamenge ameongeza kuwa amani iliyopo nchini ni tunu kubwa inayopaswa kulindwa na kila Mtanzania, hususan katika kipindi hiki cha mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.

“Amani ya Nchi yetu ni msingi wa maendeleo hivyo kila mmoja wetu ana wajibu wa kuilinda kwa vitendo na maneno, hasa wakati wa sikukuu na kuelekea mwaka mpya,” ameongeza.

Aidha, amewahimiza viongozi na Wananchi kuendeleza maadili mema, kushirikiana katika shughuli za maendeleo na kuuenzi utu wa kila Mtanzania bila kujali tofauti za kidini au kisiasa.

Ikumbukwe kuwa Evance Kamenge aliwahi kuonyesha nia ya kugombea ubunge wa Jimbo la Nkenge katika uchaguzi wa mwaka 2025, hatua iliyomfanya kuwa karibu zaidi na wananchi na kuyafahamu kwa undani changamoto za kijamii na kiuchumi zinazowakabili.

Evance  Kamenge amewatakia Watanzania wote mwaka mpya uliojaa mafanikio, afya njema na mshikamano kwa ajili ya ustawi wa taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post