" MUNGU ANAVYOMPA KIBALI NAIBU SPIKA DANIEL SILLO KUONGOZA HARAMBEE KUCHANGIA TAASISI ZA DINI

MUNGU ANAVYOMPA KIBALI NAIBU SPIKA DANIEL SILLO KUONGOZA HARAMBEE KUCHANGIA TAASISI ZA DINI


Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo, akizungumza wakati akiongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Utatu Mtakatifu Masakta, Jimbo Katoliki la Mbulu, wilayani Hanang’ mkoani Manyara Desemba 28, 2025.
..........................................

Na Dotto Mwaibale

NAIBU Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Daniel Sillo, Mungu ameendelea kumpa kibali cha kuongoza harambee za uchangiaji wa shughuli za kidini ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa.

Desemba 28, 2025 Mhe. Sillo aliongoza harambee ya kuchangia ujenzi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Utatu Mtakatifu Masakta, Jimbo Katoliki la Mbulu, wilayani Hanang’ mkoani Manyara ambapo jumla ya Sh.Milioni 37 zilipatikana.

Harambee hiyo inakuwa ya pili kuifanya tangu alipochaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya ile aliyoifanya Novemba 23, 2025 katika Kanisa la Tirano lililopo eneo la Galapo mkoani humo ambapo alichangisha Sh. Milioni 5.7 kwa ajili ya ununuzi wa vyombo vya muziki ambavyo vitatumika kuhubiri injili kwa njia ya uimbaji.

Jambo hilo katika imani siyo dogo linaonesha ni jinsi gani Mungu anavyompa kibali mtumishi wake huyo katika kufanya kazi yake ya kuwatumikia wananchi kwa namna tofauti.

Katika harambee zote hizo Mhe. Sillo amekuwa akisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika shughuli mbalimbali za maendeleo pamoja na ujenzi wa nyumba za ibada.

Aidha, jambo lingine ambalo amekuwa akilihimiza ni Watanzania kuendelea kuilinda na kudumisha amani na kueleza kuwa amani ndiyo inayowafanya watu waweze kukutana na kufanya shughuli za maendeleo na kuabudu ambapo alitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi wa dini kuendelea kumuombea Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wakiwemo wabunge.

Akizungumza katika harambee hiyo Paroko wa Parokia ya Utatu Mtakatifu Masakta, Padre Gabriel Mrina, alimshukuru Naibu Spika kwa kuitikia wito wa kuongoza tukio hilo la Baraka na kumtakia mafanikio zaidi katika kulitumikia Taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Parokia, Karoli Paulo, alisema kanisa hilo litaendelea kuhubiri amani amani na kuwakumbusha waumini wake kuendelea kuwa na maadili mema, upendo na kuheshimiana pasipo kumbagua mtu.

Katika harambee hiyo iliyohusisha michango ya waumini na wadau mbalimbali, jumla ya Sh. Milioni 37 zimepatikana na kiasi cha fedha zinazohitaji ili kukamilisha ujenzi huo ni Sh. Milioni 49.

Kanisa hilo lenye vigango saba, chini ya Mapadri wa Shirika la Utume wa Yesu, lilianza mwaka 2001 na limekuwa kitovu muhimu cha ibada na huduma za kijamii kwa waumini wa eneo la Masakta.

Baadhi ya waumini wa kanisa hilo, akiwemo Paul Andrew alisema kukamilika kwa ujenzi wa  kanisa hilo kutakuwa na tija kubwa kwa wananchi wa eneo hilo la Masakta na wilaya ya Hanang’ kwa ujumla.

Naibu Spika Mhe. Sillo akiongoza harambee hiyo.
Viongozi wa kanisa hilo wakiwa kwenye harambee hiyo.
 

Muonekano wa kanisa hilo ambalo ujenzi wake unaendelea.

Post a Comment

Previous Post Next Post