SERIKALI imesema itaendelea kuboresha miundombinu na kuongeza uwekezaji katika sekta ya utalii kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni nane ifikapo mwaka 2030, kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Pia imepanga kutatua changamoto za kikodi na zisizo za kikodi zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo, hatua itakayoboresha mazingira ya biashara na kuongeza ushindani wa sekta ya utalii nchini.
Kauli hiyo imetolewa Disemba 15, 2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Ashatu Kijaji, wakati wa hafla ya kukabidhi Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards 2025) iliyofanyika eneo la Mtumba, jijini Dodoma.
Ameielekeza Idara ya Utalii kusimamia ipasavyo utekelezaji wa sera na sheria hizo kwa lengo la kuvutia uwekezaji, kuongeza idadi ya watalii na kuimarisha mchango wa sekta ya utalii katika pato la taifa.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na kuongeza uwekezaji katika sekta ya utalii ili kuifanya Tanzania kuwa kivutio kikubwa zaidi cha utalii duniani.
Akizungumza baada ya kupokea rasmi tuzo hizo, Dkt. Kijaji amesema mafanikio hayo ni matokeo ya jitihada mahsusi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, hususan kupitia filamu ya Royal Tour iliyolitangaza Taifa kimataifa.
Ameeleza kuwa tuzo hizo, zilizotolewa katika hafla ya kimataifa iliyofanyika Desemba 6, 2025 nchini Bahrain, ni uthibitisho wa mafanikio ya sekta ya utalii na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita.
“Kupitia Royal Tour, dunia imejionea kwa macho yake utajiri wa vivutio vyetu vya asili, malikale, utamaduni pamoja na fursa za uwekezaji wa utalii,” amesema.
Ameongeza kuwa jitihada hizo zimeimarisha taswira ya Tanzania kama nchi salama, yenye amani na vivutio vya kipekee, hali iliyopelekea kuongezeka kwa idadi ya watalii, kuimarika kwa imani ya wawekezaji na kuongezeka kwa ushindani wa Tanzania katika soko la utalii duniani.
Dkt. Kijaji ameishukuru sekta binafsi kwa mchango wake katika mafanikio hayo na kuahidi kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kushirikiana na wadau wote ili kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji wa utalii.
Katika Tuzo za World Travel Awards 2025, Tanzania imeibuka kidedea kwa kushinda tuzo za World’s Leading National Park (Hifadhi ya Taifa ya Serengeti), World’s Leading Balloon Ride Operator (Serengeti Balloon Safaris), World’s Leading Exclusive Private Island (Jumeirah Thanda Island) pamoja na Africa’s Best Corporate Retreat Destination (Zanzibar).
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment