
Na Meleka Kulwa – Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, amesema kuwa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yameondoa urasimu katika utoaji wa haki nchini, baada ya mifumo ya sasa kufanya kazi kwa ufanisi na kupunguza tuhuma za rushwa kwa watumishi wasio waaminifu.
Amesema kuwa matumizi ya TEHAMA yamepunguza msongamano wa mashauri, yameongeza kukubalika kwa ushahidi wa kielektroniki pamoja na kuwezesha tathmini ya utendaji wa Mahakama na watendaji wake.
Aidha amebainisha kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ambayo imetunga sera na sheria zinazowezesha utoaji wa haki kwa kutumia TEHAMA.
Ameyasema hayo jijini Dodoma Desemba 15, 2025, wakati wa tukio la kukabidhi vifaa vya TEHAMA ikiwemo kompyuta mpakato 70 na mashine za uchapishaji (printers) kwa Wizara ya Katiba na Sheria (10), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (20), Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (20) na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (20).
Waziri huyo amesema kuwa miongoni mwa sheria zilizotungwa kuwezesha mageuzi hayo ni Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2015 pamoja na Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2007.
Amesema kuwa lengo la mageuzi ya kidijitali ni kujenga Serikali ya kisasa yenye uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi katika mazingira ya kidijitali na kutumia teknolojia kama chombo cha kuharakisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Aidha amebainisha kuwa Serikali kupitia wizara hiyo inasimamia utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali, ambapo wizara imeendelea kuratibu jitihada mbalimbali zikiwemo ujenzi na uunganishaji wa mifumo ya Serikali pamoja na utoaji wa vifaa vya TEHAMA, kwa lengo la kuhakikisha TEHAMA inaendelea kuwa nyenzo muhimu katika utoaji wa huduma na ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Amesema kuwa ugawaji wa vifaa hivyo ni muendelezo wa kuwezesha taasisi zinazotoa haki ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa wakati, kwa ufasaha na kwa tija iliyokusudiwa.
Aidha amebainisha kuwa awali Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwezeshwa kwa kupatiwa kompyuta mpakato 40, na kufanya jumla ya kompyuta mpakato 105 kugawiwa kwa taasisi hizo, pamoja na kukabidhiwa mashine mbili za uchapishaji aina ya heavy duty kwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria.
Serikali imesema kuwa imeshuhudia mapinduzi makubwa katika taasisi zinazohusika na utoaji wa haki baada ya kuanza kutumia TEHAMA katika Mahakama na Mabaraza, hali ambayo imewezesha mashauri mengi kuendeshwa kwa uharaka na ufanisi mkubwa.
Aidha amebainisha kuwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kusisitiza mageuzi ya kidijitali kama nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa.
Akizungumza katika tukio hilo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Eliakim Maswi, amesema kuwa ugawaji wa vifaa vya TEHAMA kwa taasisi za Serikali unaakisi kwa vitendo matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma kwa lengo la kuboresha uwajibikaji na kuharakisha mageuzi ya TEHAMA.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Sylvester Mwakitali, amesema kuwa wao wanatoa haki kwa kutumia TEHAMA, hivyo vifaa hivyo vitaimarisha zaidi utendaji kazi wao ukilinganisha na hali iliyokuwepo awali.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment