" SERIKALI: "Wanaozamia" Marekani ndio Chanzo cha Vikwazo vya Viza; Watanzania Waaswa Kuacha Janja-Janja

SERIKALI: "Wanaozamia" Marekani ndio Chanzo cha Vikwazo vya Viza; Watanzania Waaswa Kuacha Janja-Janja

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu vikwazo vya viza vilivyowekwa na Serikali ya Marekani, ikibainisha kuwa hatua hiyo imetokana na vitendo vya baadhi ya Watanzania kushindwa kuzingatia sheria za uhamiaji na kugeuza safari za muda kuwa za kudumu kinyume cha sheria (kuzamia).

Taarifa iliyotolewa, Desemba 17, 2025, na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesisitiza kuwa vikwazo hivyo si matokeo ya shinikizo la kisiasa au harakati za watu fulani, bali ni matokeo ya moja kwa moja ya takwimu za uvunjifu wa sheria za viza (Visa Overstays).

Ukweli wa Takwimu: Kwanini Marekani Imechukua Hatua?

Serikali imebainisha kuwa ripoti rasmi za idara ya usalama wa ndani ya Marekani zinaonyesha kuwa Watanzania wengi wamekuwa wakikaa nchini humo muda mrefu zaidi ya ule uliopangwa kisheria. Imeelezwa kuwa Viza za Matembezi na Biashara (B-1/B-2): Kiwango cha ukiukwaji kimefikia 8.3% wakati Viza za Masomo na Mashindano (F, M, J): Kiwango cha ukiukwaji ni kikubwa zaidi kikifikia 13.97%.

"Huu ni ukweli mchungu ambao Watanzania lazima wauone. Hatua ya Marekani haina uhusiano na kelele za wanaharakati wanaojaribu kujitafutia sifa mitandaoni. Hili ni suala la kisheria na utaratibu wa nchi. Tunapokwenda ugenini, ni lazima tuheshimu muda wa kukaa ulioandikwa kwenye viza," ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Onyo kwa "Wanaozamia" na Wanaharakati

Serikali imetoa onyo kali kwa watu wanaosafiri kwa kisingizio cha mambo mbalimbali kisha kutokomea nchini humo kinyume cha sheria. Vitendo hivyo vinatayarisha mazingira magumu kwa Watanzania wengine wenye uhitaji wa kweli wa matibabu, masomo, na biashara kupata viza.

Vilevile, Serikali imewataka raia kupuuza madai ya baadhi ya watu wanaojiita wanaharakati wanaodai kuwa vikwazo hivyo vimetokana na "harakati" zao. Ukweli ni kwamba nchi nyingine 11 za Afrika, ikiwemo Nigeria na Zambia, zimepewa masharti hayo hayo kutokana na changamoto kama hiyo ya raia wao kuzamia.

Hatua za Kidiplomasia

Hata hivyo, Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa tayari imeshaanza mazungumzo ya kidiplomasia na Serikali ya Rais Donald Trump ili kuweka utaratibu utakaowatofautisha wasafiri waaminifu na wale wanaokiuka sheria, kwa lengo la kuiondoa Tanzania kwenye orodha hiyo.

Wito wa Serikali: "Tanzania ni Taifa imara na lenye heshima. Watanzania wote wanaokwenda Marekani wanahimizwa kuilinda hadhi ya nchi kwa kurudi nyumbani pindi muda wao unapoisha. Tusikubali hadhi ya nchi yetu ichezewe kwa sababu ya maslahi binafsi ya watu wachache wanaotaka kusalia nchi za watu kinyume cha sheria."

Post a Comment

Previous Post Next Post