" DIPLOMASIA YA TAKWIMU: Jinsi ‘Kejeli’ za Sweden dhidi ya Tanzania zilivyozimwa

DIPLOMASIA YA TAKWIMU: Jinsi ‘Kejeli’ za Sweden dhidi ya Tanzania zilivyozimwa


Katika ulimwengu wa diplomasia, mara nyingi maneno hupimwa kwa mizani. Lakini wiki hii, Balozi wa Tanzania nchi za Nordic, Mhe. Mobhare Matinyi, ameamua kutumia lugha ambayo haina upinzani duniani: Lugha ya Takwimu. 

Hivi karibuni, Waziri wa Misaada wa Sweden, Benjamin Dousa, alitoa kauli zilizozua mjadala akidai kuwa Tanzania imekwama kwenye "Ujamaa" na haina maendeleo ya kuridhisha, akitumia hoja hiyo kuhalalisha uamuzi wa nchi hiyo kukata misaada. Hata hivyo, jibu la Balozi Matinyi kupitia gazeti la Aftonbladet limekuwa fundisho tosha la diplomasia ya kisasa.

Huu hapa ni uchambuzi wa kina wa mapigo ya takwimu yaliyotumiwa na Balozi Matinyi kuonyesha kuwa Sweden inapoteza fursa kwa kuitazama Tanzania kwa jicho la kizamani:

Mapinduzi ya Miundombinu: Kutoka "Misaada" hadi "Miradi Mikubwa"

Balozi Matinyi amepigilia msumari kwenye miradi inayofanya Tanzania kuwa kitovu kipya cha uchumi Mashariki mwa Afrika.

Mradi wa LNG (Dola Bilioni 42): 

Balozi amewakumbusha Waswidi kuwa Tanzania inajiandaa kuwa "Giant" wa nishati duniani kupitia mradi huu wa gesi asilia. Thamani ya mradi huu pekee inafanya misaada ya Sweden (SEK milioni 560) ionekane kama "vijisenti" ambavyo Tanzania inaweza kuvimudu kwa rasilimali zake.

Reli ya Umeme (SGR): 

Tanzania imekuwa nchi ya kwanza katika ukanda huu kuwa na reli ya umeme yenye kasi (electric SGR). Huku ni kuonyesha kuwa Tanzania inafanya mambo ambayo hata baadhi ya nchi zilizoendelea barani Ulaya bado zinapambana kuyakamilisha.

Ulinganifu wa Kiuchumi: Tanzania Ina "Energy" Zaidi?

Moja ya hoja nzito za Balozi ilikuwa kulinganisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania na ule wa Sweden kwa kutumia vigezo vya kimataifa:

Ukuaji wa Pato la Taifa (GDP Growth): 

Wakati Sweden ikiwa na uchumi mkubwa, Balozi ametoa dongo la kidiplomasia akibainisha kuwa Tanzania imekua kwa wastani wa 5-7% kila mwaka tangu 2000. Alizidi kuumiza pale alipoonyesha kuwa Sweden imepata ukuaji hasi (negative growth) mara mbili katika miaka mitano iliyopita.

Dhahabu vs. Misaada: 

Balozi ameweka wazi kuwa Tanzania sasa ni nchi ya biashara. Kwa kuuza dhahabu pekee, nchi inatarajia kukusanya zaidi ya Dola Bilioni 4.43, kiasi ambacho ni kikubwa mara nyingi kuliko msaada wowote unaotoka Sweden.

Maendeleo ya Jamii: Ukuaji wa 900% Sekta ya Afya

Wakati Waziri wa Sweden akidai Tanzania haina maendeleo, Balozi Matinyi alitoa takwimu za sekta ya huduma ambazo hazina ubishi:

Sekta ya Afya: 

Idadi ya vituo vya afya imeongezeka kutoka 1,343 wakati wa uhuru hadi kufikia 13,606 hivi sasa. Huu ni ukuaji wa zaidi ya 900%. Takwimu hizi zinathibitisha kuwa Serikali ya Tanzania imewekeza kwa nguvu katika utu na maendeleo ya watu wake bila kusubiri fadhila za nje.

Uchambuzi unaonyesha kuwa Waziri wa Sweden alijaribu kutumia kisingizio cha "Ujamaa" (Socialism) ili kufurahisha siasa za ndani ya nchi yake na kuhalalisha kubana matumizi.Balozi Matinyi amemvua nguo kwa kuonyesha kuwa Tanzania ya leo ni ya Soko Huria (Mixed Economy), yenye demokrasia ya vyama vingi, na miradi ya kimkakati inayozidi hata baadhi ya mataifa ya Ulaya. Jibu hili limebadili simulizi (narrative) kutoka kwa Tanzania "muombaji" na kuwa Tanzania "mshirika wa kibiashara."

Post a Comment

Previous Post Next Post