Na Fabius Clavery, Misalaba Media -Kagera.Serikali ya Mkoa wa Kagera imeandaa mkakati wa miaka mitano (5) wa kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana mkoani humo, mkakati unaotarajiwa kutengeneza nafasi za ajira takribani 16,000 kila mwaka.Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatuma Mwassa, Desemba 19, 2025, wakati akizungumza na vijana wa mkoa huo katika Kongamano la Uwekezaji lililofanyika mkoani Kagera, kongamano lililowalenga zaidi vijana na kufanyika ikiwa ni sehemu ya Tamasha la Ijuka Omuka 2025 lenye maana ya “Kumbuka Nyumbani”.Mkuu wa Mkoa amesema kuwa kila halmashauri mkoani Kagera itahakikisha inatengeneza ajira zisizopungua 2,000 kwa vijana, hatua itakayosaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira, kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, mkoa pamoja na taifa kwa ujumla.Akifafanua zaidi, Hajjat Mwassa amesema kuwa mwaka huu serikali ya mkoa imeweka mkazo mkubwa kwa vijana, akisisitiza kuwa jambo hilo si la bahati mbaya bali ni matokeo ya mipango madhubuti. Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, 2023 na 2024, mkoa ulitenga maeneo na kuanzisha miradi mbalimbali kwa ajili ya vijana katika halmashauri zake, miradi iliyofanikiwa kwa kiwango kikubwa.Ameongeza kuwa sasa lengo ni kuongeza idadi ya wanufaika, kuongeza mitaji na kupata matokeo makubwa zaidi kwa vijana wanaonufaika na miradi hiyo.Awali akiwasilisha wasilisho la Mkakati wa Uwezeshaji Vijana, mtaalam mshauri, Ndg. Adam Mbyalu, amesema mkakati huo umeainisha maeneo matatu ya kipaumbele ambayo ni kilimo, ufugaji na uvuvi, akibainisha kuwa sekta hizo zina uwezo wa kutoa matokeo ya haraka katika kuwawezesha vijana kiuchumi.Ameongeza kuwa mkakati huo unaelekeza mabadiliko kutoka kuwapa vijana mafunzo pekee na kuwajengea makongani, kwenda katika kufadhili huduma za biashara, shughuli maalum za kiuchumi pamoja na kutoa vifaa. Aidha, mkakati unasisitiza serikali kufanya kazi kwa mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), kuwezesha vijana kuanzisha na kujiunga na SACCOS zao, pamoja na kufungua na kuendeleza maeneo ya uwekezaji.Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Vijana, Dkt. Kedmon Mapana, ameupongeza Mkoa wa Kagera kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kuwawezesha vijana ikiwemo uanzishaji wa makongani, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia mitandao ya kijamii kutangaza fursa zinazopatikana.Mapema akizungumza katika kongamano hilo, Mkurugenzi wa KADERES, Bw. Leonard Faustine Kachebonaho, amesema taasisi zake zitaendelea kushirikiana na serikali kwa kuwapatia vijana fursa mbalimbali zitakazowawezesha kuinuka kiuchumi.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Hajjat Fatuma Mwassa akizungumza.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Vijana, Dkt. Kedmon Mapana akizungumza.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment