" SHIRIKA LA JOSEPH MUHUNDA NYERERE FOUNDATION NA YOUTH VOCATIONAL DEVELOPMENT AND TRANSFORMATION WAKUTANA NA SERIKALI KUJADILI MASUALA YA MAZINGIRA

SHIRIKA LA JOSEPH MUHUNDA NYERERE FOUNDATION NA YOUTH VOCATIONAL DEVELOPMENT AND TRANSFORMATION WAKUTANA NA SERIKALI KUJADILI MASUALA YA MAZINGIRA


Shirika ya Joseph Muhunda Nyerere Foundation (JMN Foundation) na Youth VDT (Youth – Vocational Development and Transformation) leo Disemba 17, 2025 yamefanya kikao cha pamoja na Afisa Maliasili na Mazingira wa Manispaa ya Shinyanga, Mwl. Ezra Manjerenga, kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

Katika kikao hicho, washiriki walijadili kwa kina mikakati ya kulinda mazingira ikiwemo upandaji wa miti, utunzaji wa rasilimali asilia, pamoja na kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika shughuli za uhifadhi wa mazingira kwa maendeleo endelevu ya Manispaa ya Shinyanga.

Afisa Maliasili na Mazingira, Mwl. Ezra Manjerenga, amebainisha kuwa licha ya kuwepo kwa juhudi mbalimbali za serikali na wadau, elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira bado ni changamoto kubwa, hali inayosababisha uharibifu wa mazingira kuendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo.

Kwa upande wao, viongozi wa mashirika hayo mawili wamesisitiza kuwa ushirikiano kati ya serikali na mashirika ya kiraia ni muhimu katika kufanikisha malengo ya uhifadhi wa mazingira. 

Mratibu wa shirika la JMN Foundation Manispaa ya Shinyanga Mwalimu Leonard Mapolu, amesema kuwa shirika hilo lenye kauli mbiu isemayo “Let Us Make the World Happy”, limejipanga kuendelea kushiriki katika kampeni za uelimishaji na vitendo vya moja kwa moja kama upandaji wa miti na kutoa elimu kwa jamii.

Aidha, kupitia kampeni yao ya Shinyanga yenye kauli mbiu “Uzalendo na Mazingira Shinyanga, kwa pamoja tunaweza”, mashirika hayo yameeleza dhamira yao ya kuhamasisha uzalendo wa kweli kwa vitendo kwa kulinda mazingira kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa wake mratibu wa shirika la Youth VDT (Youth – Vocational Development and Transformation) Bwana Nicholaus Luhende, amesema shirika hilo limeeleza kuwa litaendelea kuwajengea uwezo vijana kwa kuwahusisha katika utunzaji wa mazingira, ili wawe chachu ya mabadiliko chanya katika jamii.

Kikao hicho kimehitimishwa kwa pande zote kukubaliana kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha juhudi za utunzaji wa mazingira zinakuwa endelevu na zenye manufaa kwa wananchi wa Shinyanga kwa ujumla.

Post a Comment

Previous Post Next Post