" TANZANIA YAENDELEZA DESTURI YA KUSITISHA SHEREHE ZA UHURU NA KUELEKEZA FEDHA KWENYE HUDUMA ZA JAMII

TANZANIA YAENDELEZA DESTURI YA KUSITISHA SHEREHE ZA UHURU NA KUELEKEZA FEDHA KWENYE HUDUMA ZA JAMII


Tanzania ilivyobadilisha kusheherekea sherehe za uhuru katika miaka kumi kutoka mwaka 2015 hadi mwaka 2025 zimeahirishwa mara 6, huku fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya madhimisho ya sherehe hizo zikipelekwa kufanya kazi za kusaidia huduma za jamii nchini.

Wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, Samia Suluhu Hassan alipotangaza Novemba 24, 2025 kuwa maadhimisho ya Uhuru wa Tanzania Bara yamesitishwa mwaka huu, fedha zilizotengwa zilielekezwa katika ukarabati wa miundombinu ya umma iliyoharibiwa wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025.

Hii ilikuwa mara ya tatu tangu aingie madarakani Machi 21 mwaka 2021 kuchukua uamuzi kama huo, hatua inayoendeleza utamaduni ulioanzishwa na mtangulizi wake, hayati Rais Dkt, John Pombe Magufuli, ambaye naye mara kadhaa alisitisha sherehe za kitaifa ili kutoa kipaumbele kwa mahitaji ya dharura ya wananchi kuliko shamrashamra za kitaifa.

Kwa nchi iliyozoea gwaride la kijeshi, maonesho ya kitamaduni na dhifa za kitaifa kila tarehe 9 Desemba, marudio ya kusitishwa kwa sherehe hizo yanaashiria mabadiliko ya namna maadhimisho hayo yanavyoonekana.

Taratibu, maadhimisho chini ya utawala wa sasa yamegeukia kwenye huduma za jamii, maendeleo na tafakuri ya wajibu wa pamoja badala ya shamrashamra za kijeshi na tamasha.

Siku ya Uhuru inazidi kuwa siku si ya kukumbuka historia pekee, bali kuonesha dhamira ya kuendeleza ustawi wa jamii, yaani Kazi na Utu, Tunasonga Mbele.

Mabadiliko ya kwanza makubwa yalitokea Desemba mwaka 2022, chini ya mwaka mmoja tangu aingie madarakani.

Serikali ilitangaza kuwa hakutakuwa na maadhimisho ya kitaifa, na badala fedha zilizotengwa zipelekwe kujenga mabweni kwa wanafunzi wenye uhitaji maalumu nchini.

Serikali za mikoa na wilaya ziliagizwa kuadhimisha siku hiyo kwa miradi ya kijamii na shughuli za maendeleo.

Uamuzi huo uliibua pongezi nyingi ukidhihirisha uongozi wa Rais Dkt, Samia unaozingatia uhalisia na mahitaji ya wananchi, huku ukidumisha urithi wa Magufuli wa kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Desemba 4 mwaka 2024, sherehe za Uhuru zilisitishwa tena, na taasisi za umma zikaelekezwa kuelekeza fedha zilizotengwa kufanya huduma za kijamii.

Waziri Mkuu wa wakati huo, Kassim Majaliwa, alisema “kila mkoa na wilaya itafanya usafi wa mazingira, kupanda miti, kusaidia hospitali na kushiriki katika shughuli zinazowanufaisha wananchi moja kwa moja.”

Kwa wakati huo, tafakuri ya kitaifa ilikuwa imehamia hospitalini, mitaani, shuleni na sokoni.

Aidha, kusitishwa kwa sherehe za mwaka huu kulikumbwa na mazingira tofauti, nchi ilikuwa bado inaponya majeraha ya vurugu za Oktoba 29 zilizotoa vifo, majeruhi, uharibifu wa mali na kuharibu miundombinu ikiwemo mfumo wa mabasi ya mwendokasi.

Wakati akitembelea maeneo yaliyoathirika jijini Dar es salaam, Waziri Mkuu, mpya Dkt, Mwigulu Nchemba, alitangaza agizo la Rais: hakuna maadhimisho ya Uhuru, fedha zielekezwe moja kwa moja kurekebisha miundombinu na kurejesha huduma.

Aliwataka wananchi kushiriki katika ujenzi na akatahadharisha kuhusu uchochezi kutoka nje, “Wanaochochea vurugu kutoka nje hawajali mateso ya Watanzania wa kawaida.”

Pia aliwataka vijana kutumia Wizara mpya ya Maendeleo ya Vijana kutatua changamoto zao kwa njia za kimaendeleo.

Mwaka huu 2025, Tanzania Bara inatimiza miaka 64 ya Uhuru tangu ilipopata uhuru wake mwaka 1961.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post