" UMKI YAMSHUKURU KAMENGE KWA MCHANGO MKUBWA WA MAENDELEO

UMKI YAMSHUKURU KAMENGE KWA MCHANGO MKUBWA WA MAENDELEO


Na Lydia Lugakila -Misalaba media MissenyiKatibu wa Umoja wa Maendeleo Kikukwe (UMKI), Bi. Magreth Kyai, amempongeza na kumshukuru mchumi na mchambuzi wa masuala ya siasa, Evance Kamenge, kwa kutoa mchango wa shilingi milioni moja, akimtaja kuwa ni kijana wa mfano, mzalendo na mwenye moyo wa kujitolea kwa vitendo katika kugusa maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo ya jamii.Bi. Magreth amesema mchango wa Kamenge unaonesha uhalisia wa uzalendo na uwajibikaji kwa jamii, akibainisha kuwa amekuwa mdau muhimu anayeshirikiana vyema na wadau mbalimbali wa maendeleo katika ngazi ya wilaya na mkoa kwa ujumla.Ameongeza kuwa Umoja wa Maendeleo Kikukwe (UMKI), tangu kuanzishwa kwake, umefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, na kwa sasa upo katika hatua za mwisho za kukamilisha bweni la kulala wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Kikukwe kwa kushirikiana na Serikali.Kwa mujibu wa Bi. Magreth, bweni hilo linatarajiwa kuhudumia wanafunzi zaidi ya 70, jambo litakalosaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya elimu na kuongeza fursa za masomo kwa watoto wa kike katika kijiji hicho na maeneo ya jirani.Kwa upande wake, Evance Kamenge amewahimiza wananchi wenye uwezo kushiriki kikamilifu katika kusaidia jamii kwa kushirikiana na UMKI, akisisitiza kuwa maendeleo endelevu yanapatikana kupitia mshikamano na ushirikiano wa pamoja, si juhudi za mtu mmoja.Kamenge ameeleza kuwa kati ya fedha alizochangia, shilingi laki saba zimetengwa kwa ajili ya kusaidia miradi ya maendeleo ya kijiji, huku shilingi laki tatu zikielekezwa kama zawadi kwa washindi wa mashindano ya mpira wa miguu ya ligi ya vitongoji iliyokuwa ikiendelea katika Kijiji cha Kikukwe.Amesema ameamua kutoa mchango huo baada ya kuvutiwa na juhudi, mshikamano na uwajibikaji unaoonyeshwa na UMKI katika kuwahudumia wananchi wasiojiweza na kusukuma mbele maendeleo ya kijiji hicho.Mchango huo umetolewa Desemba 27, 2025, wakati wa Tamasha la Maendeleo Kikukwe (Kikukwe Day), ambapo Evance Kamenge alikuwa mgeni rasmi katika tukio lililofanyika Kijiji cha Kikukwe, Kata ya Kanyigo, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera.Hata hivyo Kamenge amekuwa akiwavutia watu wengi katika Mkoa wa Kagera kutokana na kutojivuna pia kuwa na moyo wa kuwasaidia wasiojiweza ambapo ndoto yake ni kufanya mengi zaidi ikiwa ni kusaidia jamii zaidi.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post