" GEITA: SMAUJATA TAIFA YAANZISHA RASMI KAMPENI YA “SMAUJATA NA MAZINGIRA” YA MIEZI TISA

GEITA: SMAUJATA TAIFA YAANZISHA RASMI KAMPENI YA “SMAUJATA NA MAZINGIRA” YA MIEZI TISA

Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira wa SMAUJATA Taifa, Shujaa Eng. Shadya Jamali, yupo mkoani Geita katika ziara ya kikazi inayolenga uzinduzi na utekelezaji wa Kampeni ya SMAUJATA na Mazingira, kampeni inayotarajiwa kuendelea kwa muda wa miezi tisa kuanzia tarehe 20 mwezi huu, mwaka 2025.

Kampeni hiyo inayofanyika chini ya kaulimbiu ya “Tanzania ni Mazingira” inalenga kipindi cha masika na maeneo ya mabonde yenye unyevunyevu, ikiwa ni sehemu ya Operesheni Maalum ya uhifadhi wa mazingira kupitia upandaji miti na elimu kwa jamii.

Katika zoezi hilo, uongozi wa SMAUJATA Mkoa wa Geita unashiriki kikamilifu kwa kupanda miti katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, ukiongozwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira SMAUJATA Taifa, Shujaa Eng. Shadya Jamali, Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Geita, Shujaa Ndg. Jastine Stanslaus Katunzi, pamoja na Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Geita, Shujaa Ndg. Amos Samwel Magige.

Akizungumza na wanachama na wananchi wa Geita, Shujaa Eng. Shadya Jamali amesisitiza kuwa suala la mazingira ni wajibu wa kila mmoja, akieleza umuhimu wa kulinda rasilimali zilizopo mkoani humo.

“Ndugu mashujaa wa SMAUJATA Mkoa wa Geita, suala la mazingira ni jukumu letu sote. Geita ni mkoa wenye rasilimali nyingi—ardhi, misitu, maji na madini—lakini rasilimali hizi zinaendelea kuathirika kutokana na ukataji miti hovyo, uchimbaji usiozingatia mazingira na uchafuzi wa vyanzo vya maji.

SMAUJATA Taifa tunahimiza kila mwananchi kuwa mlinzi wa mazingira kwa kupanda miti, kutunza vyanzo vya maji, kudhibiti uchafu na kuzingatia sheria za mazingira. Kulinda mazingira leo ni kulinda afya, uchumi na maisha ya kizazi cha sasa na kijacho. Tuungane, tushirikiane na serikali katika kulinda na kutunza mazingira ya Geita na Taifa kwa ujumla.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Geita, Shujaa Ndg. Jastine Stanslaus Katunzi, anatumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kupinga ukatili katika jamii, akieleza kuwa ukatili ni changamoto inayodhoofisha ustawi wa familia na maendeleo ya taifa.

“Ndugu wananchi wa Mkoa wa Geita, ukatili ni tatizo kubwa linaloathiri familia, jamii na maendeleo ya taifa letu. Ukatili unaweza kuwa wa kimwili, kisaikolojia, kingono au kiuchumi, na mara nyingi huathiri wanawake, watoto na hata wanaume.

SMAUJATA tunatoa wito kwa kila mmoja wetu kupinga ukatili kwa vitendo, kutoa taarifa mapema, na kulinda haki na utu wa kila mwananchi. Jamii yenye amani hujengwa kwa upendo, heshima na mshikamano. Tushirikiane sote kutokomeza ukatili ili kujenga Geita salama na yenye maendeleo.”

Naye Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Geita, Shujaa Ndg. Amos Samwel Magige, anakazia zaidi suala la ukatili wa kijinsia, akieleza kuwa ni kosa la kisheria na kinyume na maadili ya jamii.

Amewahimiza wananchi kuacha ukimya, kutoa taarifa mapema juu ya vitendo vya ukatili na kushirikiana na viongozi pamoja na vyombo vya dola katika kulinda wanawake, watoto na makundi yote yaliyo katika hatari, huku akisisitiza elimu, heshima na usawa wa kijinsia kama msingi wa kumaliza kabisa ukatili katika jamii.

Kampeni ya SMAUJATA na Mazingira inaendelea mkoani Geita ikiwa na lengo la kuhamasisha uhifadhi wa mazingira sambamba na kujenga jamii yenye maadili, amani na mshikamano.

“HEKIMA NA UMOJA USHINDI NA USHUJAA” 🇹🇿💪🏿

 

Post a Comment

Previous Post Next Post