" 1200 WAJITOKEZA KUPATA TIBA KAMBI YA MATIBABU YA MOYO ARUSHA CHINI YA JKCI

1200 WAJITOKEZA KUPATA TIBA KAMBI YA MATIBABU YA MOYO ARUSHA CHINI YA JKCI

Na Seif Mangwangi, Arusha

ZAIDI ya wananchi 1200 wamejitokeza kupata huduma ya bure ya matibabu ya moyo katika Kambi iliyowekwa katika hospitali ya Seliani Jijini Arusha kwa ushirikiano wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Hospitali ya Arusha Lutheran Centre (Seliani).


Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amosi Makalla ameyasema hayo leo 6 Januari 2026 alipotembelea Kambi hiyo na kuzungumza na madaktari pamoja na wananchi wanaoendelea kupata tiba.

Amesema Kambi hiyo mbali ya kuwa msaada kwa wananchi wa Arusha na Mikoa ya jirani lakini pia itasaidia wageni wote watakaotembelea Arusha kushuhudia michuano ya Ampira wa miguu  AFCON mwaka 2027.

CPA Makalla amesema ujenzi wa Kituo cha JKCI katika Hospitali hiyo kutasaidia pia wananchi, watalii pamoja na washiriki wa michuano ya Mpira wa miguu kwa mataifa huru ya Afrika (AFCON) itakayochezwa Mkoani Arusha mwaka 2027.

Aidha CPA Makalla amesema  serikali itawawezesha wananchi wasiokuwa na uwezo na waliopewa rufaa ya kwenda kutibiwa zaidi kwenye Taasisi ya Moyo JKCI Mkoani Dar Es Salaam.

“Magonjwa ya moyo yanahitaji uchunguzi wa mapema na matibabu ya haraka. Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma hizi bila kikwazo chochote, hususan kwa wale wasio na uwezo wa kugharamia matibabu,” alisema Makalla.

Wakati huo huo, CPA Makalla amewataka wananchi wa Arusha kujiunga na mfumo wa Bima Kwa wote Ili waweze kupata huduma za uhakika za matibabu.

Wananchi kwa upande wao wamemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwezeshaji wake wa programu ya vipimo na matibabu bure kwa magonjwa ya moyo.



 

Post a Comment

Previous Post Next Post