Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera.
Baadhi ya madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera wamesema kuwa licha ya Serikali kuendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo baadhi ya wazazi kutotoa kipaumbele cha kutosha kwa suala la elimu, hali inayosababisha baadhi ya watoto kuchelewa kuanza masomo kwa wakati.
Wakizungumza na waandishi wa habari,Hamimilu Byeyombo Diwani wa Kata ya Kanyangereko,Jasson Rwankomezi Diwani wakata ya Kaibanja,Severiani Kijoma mwenyekiti kamati ya Elimu Afya na Maji,pamoja na Julias Rweyemamu Diwani wa kata ya Rubale,wamesema kuwa kwa sasa wanaendelea kuhamasisha na kuelimisha wazazi kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na Kidato cha Kwanza wanapelekwa shuleni kwa wakati, sambamba na watoto wenye sifa ya kuanza Darasa la Kwanza na elimu ya awali.
Madiwani hao wameeleza kuwa juhudi hizo zinafanyika kupitia mikutano mbalimbali ya kijamii, ambapo wanawahamasisha wazazi juu ya umuhimu wa elimu na kuwahimiza kushirikiana na serikali katika kukabiliana na changamoto chache zilizopo shuleni, wakati serikali ikiendelea kushughulikia changamoto hizo kwa ujumla.
Kwa upande wake, mhe.Sadoth Ijunga Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo amekemea baadhi ya wanafunzi wanaojihusisha na vitendo vya utovu wa nidhamu na maadili, akiwataka kuacha mara moja tabia hizo na kuzingatia masomo yao, akisema kuwa lengo kuu la uwepo wao shuleni ni kujijengea msingi imara wa maisha yao ya baadaye.
Awali, akihutubia kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Erasto Siima, amewataka madiwani kufuatilia kwa karibu mwenendo wa uandikishaji wa wanafunzi katika shule zilizopo kwenye kata zao na kuhakikisha hakuna vikwazo vyovyote vinavyotokana na upande wa utawala.
Aidha, Mkuu wa Wilaya amewataka wazazi ambao bado hawajawapeleka watoto wao shuleni kufanya hivyo mara moja ili kuepuka msako unaotarajiwa kuanza hivi karibuni. Ameeleza kuwa zoezi la uandikishaji wa wanafunzi wa Darasa la Kwanza, elimu ya awali na Kidato cha Kwanza bado lipo katika asilimia 80 tangu kufunguliwa kwa muhula mpya wa masomo Januari 13 mwaka huu.


Post a Comment