Na:Mbeki Mbeki
Kagera.
Bodi ya Brute SACCOs inayopatikana katika Manispaa ya Bukoba imeendesha mafunzo ya uandishi wa habari kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi na wanachama wake kuandika habari zenye maslahi kwa ajili ya kuitangaza SACCO yao na shughuli zake kwa umma.
Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa KCU, Manispaa ya Bukoba, yakihusisha wajumbe wa bodi na wanachama wake wakiongozwa na Mwenyekiti wa Brute SACCOs, Charles Tegamaisho, pamoja na mshiriki Joseline Kyaruzi, ambapo washiriki walieleza kuwa lengo kuu la kujifunza uandishi wa habari ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu huduma, mafanikio na mchango wa Brute SACCOs katika maendeleo ya kiuchumi ya wanachama wake.
Katika mafunzo hayo, washiriki walijifunza mambo ya msingi katika uandishi wa habari, yakiwemo kuelewa habari ni nini, na vigezo vinavyofanya tukio au taarifa kuitwa habari. Aidha, walijifunza aina mbalimbali za habari, zikiwemo habari za kawaida (straight news), habari za makala (feature stories), habari za maendeleo na habari za maslahi ya jamii.
Washiriki pia walipata elimu kuhusu sababu za kuandika habari, hususan umuhimu wa kutoa taarifa sahihi, kuelimisha jamii, kujenga taswira chanya ya taasisi na kuvutia wanachama wapya. Vilevile, walijifunza kwa kina kuhusu lead (utangulizi wa habari), ikiwa ni pamoja na namna ya kuandika utangulizi unaovutia na unaojibu maswali ya msingi ya habari kama nani, nini, wapi, lini, kwa nini na vipi.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, mmoja wa washiriki, Mwalimu Valence Mandoro, alisema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, hususan vipengele vinavyozuia kufanya baadhi ya vitendo vya mtandaoni ambavyo ni makosa ya jinai kikatiba.
“Tumepata ufahamu mpana kuhusu sheria hizi, jambo litakalotusaidia kuandika na kusambaza habari kwa uangalifu, kwa kuzingatia sheria, maadili na usalama wa taasisi yetu,” alisema Mandoro.
Aidha, aliongeza kuwa washiriki wamejifunza umuhimu wa kuzingatia kanuni ya 5Ws and H (Who, What, Where, When, Why and How) katika uandishi wa habari, ambayo itawasaidia kuandaa habari zilizo kamili, zenye mvuto na zenye kuleta matokeo chanya kwa jamii na kwa Brute SACCOs kwa ujumla.
Mafunzo hayo yaligusa pia misingi ya uandishi wa habari, ikiwemo matumizi sahihi ya lugha, uwazi, ukweli, uwiano na maadili ya uandishi. Sambamba na hilo, walifundishwa misingi ya habari, ikijumuisha usahihi wa taarifa, uthibitishaji wa vyanzo (fact-checking) na kuepuka upendeleo katika uandishi.
Kwa ujumla, mafunzo hayo yanatarajiwa kusaidia Brute SACCOs kuimarisha mawasiliano yake na jamii, kuongeza uwazi katika utoaji wa taarifa na kujiimarisha zaidi katika ushindani wa sekta ya vyama vya ushirika wa akiba na mikopo.
Mwenyekiti wa Brute saccos Charles Tegamaisho akiwa kwenye mafunzo.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment