" BOT YAFAFANUA UKWELI KUHUSU HIFADHI YA DHAHABU NA MWELEKEO WA UCHUMI

BOT YAFAFANUA UKWELI KUHUSU HIFADHI YA DHAHABU NA MWELEKEO WA UCHUMI

Benki Kuu ya Tanzania imetoa ufafanuzi wa kina kuhusu hatua yake ya hivi karibuni ya kusawazisha hifadhi ya dhahabu ili kukomesha upotoshaji unaosambaa mitandaoni ukidai kuwa rasilimali hiyo inauzwa kwa ajili ya kufadhili miradi ya kimkakati ya serikali. 

Mkurugenzi wa Idara ya Masoko ya Fedha wa Benki Kuu, Emmanuel Akaro amebainisha kuwa madai hayo si ya kweli na kwamba kinachotekelezwa ni mpango wa kitaalamu wa kuuza dhahabu iliyozidi kiwango kilichoidhinishwa na bodi kwa lengo la kusawazisha mizania ya hifadhi ya benki hiyo.

Akifafanua zaidi kuhusu hatua hiyo Akaro ameeleza kuwa bodi ya Benki Kuu iliidhinisha benki kuwa na hifadhi ya dhahabu isiyozidi dola za Marekani bilioni mbili lakini kutokana na mabadiliko ya thamani katika soko la dunia kiwango hicho kimefikia dola bilioni tatu nukta mbili nne. Hali hiyo imesababisha Benki Kuu kupanga kuuza kiasi hicho kilichozidi ili fedha zitakazopatikana ziwekezwe katika masoko ya fedha ya kimataifa kwa lengo la kuongeza mapato ya uwekezaji kupitia riba na si kwa ajili ya matumizi ya miradi ya serikali kama inavyovumishwa.

Uamuzi huo wa kusawazisha hifadhi unalenga pia kudhibiti hatari ya kuwekeza kupita kiasi katika aina moja ya mali kwani kutegemea dhahabu pekee kunaweza kuleta hasara endapo bei yake itashuka ghafla katika masoko ya kimataifa. Hatua hii inasaidia kueneza hatari hizo na kulinda thamani ya akiba ya taifa dhidi ya mishtuko ya kiuchumi huku ikiongeza ukwasi wa hifadhi za fedha za kigeni ambao ni muhimu katika kukabiliana na mahitaji ya haraka ya huduma za kijamii na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Benki Kuu imesisitiza kuwa yenyewe ni chombo huru na uamuzi wowote wa kutumia uwekezaji wake kufadhili miradi ya serikali unahitaji idhini ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Januari 2026, Benki Kuu ilikuwa na akiba ya fedha za kigeni yenye thamani ya dola bilioni sita nukta tano mbili ambapo kati ya hizo dhahabu inakadiriwa kuwa dola bilioni moja nukta mbili huku dola za Marekani zikiwa bilioni tatu nukta nane na sarafu ya China yuan ikiwa ni milioni mia saba thelathini na tano.

Mageuzi haya ya kiuchumi yanaashiria ukomavu wa sera za kifedha nchini Tanzania ambayo sasa inaingia kwenye orodha ya mataifa kumi bora barani Afrika yenye akiba kubwa ya dhahabu. 

Hatua hiyo imewezesha nchi kukusanya zaidi ya tani 1.7 za dhahabu chini ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan jambo ambalo linaimarisha ustahimilivu wa uchumi wa sasa na wa baadaye dhidi ya changamoto za soko la kimataifa.


Post a Comment

Previous Post Next Post