" CHILOMBE: CHANGAMOTO SUGU YA KUKATIKA UMEME TUNDURU YAENDA KUWA HISTORIA

CHILOMBE: CHANGAMOTO SUGU YA KUKATIKA UMEME TUNDURU YAENDA KUWA HISTORIA

Changamoto ya kukatika mara kwa mara kwa umeme wilayani Tunduru kwa miaka mingi imekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya kijamii, uchumi na uwekezaji, hali iliyoathiri utoaji wa huduma muhimu kama afya, elimu na shughuli za uzalishaji mali kwa wananchi.

Kwa upande wa uchumi, upungufu wa umeme wa uhakika umeathiri biashara ndogo na za kati, viwanda vidogo pamoja na wajasiriamali, huku kwa upande wa uwekezaji hali hiyo ikiifanya Tunduru kushindwa kunufaika ipasavyo na fursa za maendeleo licha ya kuwa na rasilimali za kutosha.

Hata hivyo, changamoto hiyo sasa inaelekea kuwa historia kufuatia utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi wa kituo cha kupooza umeme pamoja na ujenzi wa laini ya umeme kutoka Songea hadi Tunduru.

Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, Mhandisi Fadhili Chilombe, leo amefanya ukaguzi wa mradi huo pamoja na eneo la kuhifadhia vifaa (yard) vinavyotumika katika ujenzi wa miundombinu ya umeme.

Katika ukaguzi huo, imeelezwa kuwa takribani asilimia 95 ya vifaa vya ujenzi wa laini ya umeme yenye urefu wa kilometa 214 tayari vimefika katika maeneo ya kazi (sites), huku asilimia 99.9 ya vifaa vya kituo cha kupooza umeme vikiwa tayari vimewasili, ikiwemo transfoma (transformer).

Mhandisi Chilombe amesema ukaguzi huo umelenga kujiridhisha na hatua ya utekelezaji wa mradi, ambapo kwa ujumla mradi unaendelea vizuri na Serikali inaendelea kushughulikia masuala machache yaliyosalia ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Amesema kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kupoza na kusambaza umeme wa megawati 120, wakati mahitaji ya sasa ya Wilaya ya Tunduru ni megawati 4 pekee, hali itakayowezesha kuwepo kwa ziada ya umeme kwa ajili ya uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi.

Mbunge huyo amesisitiza kuwa wao kama wawakilishi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika jimbo hilo watahakikisha mradi unasimamiwa kwa viwango vinavyotakiwa hadi kukamilika kwake, akieleza kuwa huo ndio msingi wa kuifungua Tunduru kwa vitendo.

  

Post a Comment

Previous Post Next Post