Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew, ametoa agizo kwa viongozi wa sekta ya maji mkoani Kagera kuhakikisha kuwa wateja wote wanafungiwa dira za maji za malipo kabla (prepaid meters) ndani ya kipindi cha miezi minne, bila kuwatoza gharama yoyote.
Mhe. Kundo ametoa agizo hilo wakati akizungumza katika kikao kazi na viongozi wa sekta ya maji mkoani humo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya maboresho ya huduma ya maji na kipimo muhimu cha kupima uwajibikaji na utendaji wa viongozi katika kuwahudumia wananchi.
Ameeleza kuwa taasisi zote za umma na binafsi, hoteli, maeneo ya jumuia, pamoja na viongozi wa chama na Serikali, wanapaswa kuhakikisha wanafungiwa dira hizo ndani ya muda uliopangwa ili kuongeza uwazi katika matumizi ya maji na kuimarisha ukusanyaji wa mapato katika sekta hiyo.
Naibu Waziri amebainisha kuwa agizo hilo linatokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, yanayolenga kuifanya nchi iachane na mfumo wa matumizi ya dira za malipo baada (postpaid) na kuanza kutumia teknolojia ya kisasa ya malipo kabla, kwa lengo la kuongeza ufanisi na kudhibiti upotevu wa mapato.
Aidha, Mhe. Kundo amezitaka Bodi za Maji za Mabonde nchini kufanya tathmini ya kina ya mienendo ya vyanzo vya maji, ili kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto ya upungufu wa maji na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa huduma hiyo muhimu kwa wananchi.
Kwa sasa, Naibu Waziri wa Maji yupo mkoani Kagera kwa ziara ya kikazi inayolenga kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji pamoja na kuhimiza uwajibikaji na usimamizi bora wa rasilimali maji nchini.




Post a Comment