" KUTOKA DARASANI HADI KWENYE DHAHABU: VIJANA CHANGAMKIENI MAPINDUZI YA UJUZI YA TISEZA MKOANI GEITA

KUTOKA DARASANI HADI KWENYE DHAHABU: VIJANA CHANGAMKIENI MAPINDUZI YA UJUZI YA TISEZA MKOANI GEITA

 Wakati wasomi wengi nchini wakilalamika kuhusu uhaba wa ajira, mkoani Geita kuna dirisha la fursa ambalo limefunguliwa na Mamlaka ya Uwekezaji inayosimamia Maeneo Maalum ya Kiuchumi (TISEZA). 

Taarifa ya hivi karibuni kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, na Mwenyekiti wa Bodi ya TISEZA, Balozi Aziz Mlima, si tu habari kwa wafanyabiashara, bali ni wito wa kijasiri kwa vijana wa vyuo vya ufundi (VETA) na Vyuo Vikuu nchini.

Mwisho wa "Nguvu za Mikono", Mwanzo wa "Nguvu ya Akili" Kwa miaka mingi, kilio cha wachimbaji wadogo kimekuwa ni ukosefu na kuwa na vifaa duni. Lakini kupitia TISEZA, wawekezaji wa ndani sasa wanaingiza mitambo ya kisasa kwa gharama nafuu baada ya kuondolewa kodi. 

Hapa ndipo fursa ya kijana msomi ilipo. Mitambo hii ya kisasa haitaji "nguvu za kishamba"; inahitaji wataalamu wa mifumo ya kielektroniki, mafundi mitambo waliosomea teknolojia ya kisasa, na wataalamu wa madini wanaojua kutumia programu za kompyuta (software) kusoma miamba. Huu ni wakati wa vijana wa VETA na vyuo vya uhandisi kuacha kusoma kwa ajili ya kupata cheti tu, na kuanza kusoma kwa ajili ya kumudu mitambo hii inayomiminika Geita.

Geita haihitaji mafundi pekee kwani ukuaji wa sekta ya hoteli unaochochewa na TISEZA unahitaji wataalamu wa usimamizi wa biashara, wataalamu wa masoko, na mabingwa wa huduma za ukarimu. Kwa mwanafunzi anayesoma Utalii au Uhasibu, Geita si mkoa wa vumbi tena, bali ni soko la ajira linalohitaji utaalamu wako ili kuendesha miradi ya wawekezaji wa ndani ambao sasa wanatanua mitaji yao.

Lengo la TISEZA la kufikisha asilimia 55 ya wawekezaji wa ndani ni ishara kuwa serikali inatandika jamvi kwa ajili ya Watanzania. Hii ni changamoto kwa vijana wasomi: Badala ya kuwaza tu kuandika barua za maombi ya kazi, kwa nini usitumie utaalamu wako na wenzako wawili au watatu, mkasajili kampuni ya kutoa huduma za kiufundi au ushauri na kunufaika na misamaha ya kodi ya TISEZA? Sera hizi zipo ili kugeuza ujuzi wenu kuwa mtaji.

Mazingira ya sasa nchini Tanzania yanaonesha kuwa mnyororo wa amani, sera rafiki, na ukuzaji ujuzi umekutana mahali pamoja. Vijana msisubiri ajira ziwafuate mikoani kwenu; fuateni fursa kule ambako serikali imeweka motisha. Geita sasa ni maabara ya ufundi na ujasiriamali.

Elimu mliyoipata vyuoni ndiyo ufunguo wa kufungua kufuli za TISEZA. Ulezi wa amani uliopo nchini unatupa utulivu wa kufikiri na kuvumbua. Hivyo, acheni masikhara na masomo yenu; mkoa wa Geita unawasubiri mkaendeshe mitambo, mkasimamie hoteli, na mkawe sehemu ya asilimia 55 ya wamiliki wa uchumi wa Tanzania.

mwisho

 

Post a Comment

Previous Post Next Post