" MAKATIBU WA JUMUIYA YA WAZAZI CCM MPANDA WAPATA MWELEKEO MPYA WA KAZI 2026

MAKATIBU WA JUMUIYA YA WAZAZI CCM MPANDA WAPATA MWELEKEO MPYA WA KAZI 2026


Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Ndg. Jimotoli Jilala Maduka, tarehe 10 Januari 2026, ameongoza kikao kazi cha dharura kilichowakutanisha makatibu wa kata wa Jumuiya ya Wazazi CCM wilayani humo kwa lengo la kutoa maelekezo ya utekelezaji wa majukumu yao kwa mwaka 2026.

Katika kikao hicho, Ndg. Maduka amewahimiza makatibu wa kata kuongeza ufanisi, bidii na juhudi katika kazi za Jumuiya pamoja na kuimarisha mshikamano na umoja ndani ya chama, akisisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa ushirikiano ili kukiimarisha chama katika ngazi zote.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kusajili wanachama wapya wengi zaidi, kutoa hamasa kwa wanachama kushiriki kikamilifu katika shughuli za chama pamoja na kulipa ada kwa hiari kama sehemu ya kukijenga chama kiuchumi na kiutendaji.

Ndg. Maduka ameelekeza makatibu wote wa kata kwenda chini kwa wananchi kuhamasisha utekelezaji wa majukumu ya Jumuiya kwa mwaka 2026, huku akiwataka wajumbe na wanachama kutambua wajibu wao na kuutekeleza ipasavyo kwa maendeleo ya Jumuiya na chama kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Katibu huyo ameagiza kila kata kubuni miradi mbalimbali ya kiuchumi ya Jumuiya ya Wazazi CCM kwa lengo la kuongeza kipato na kuchochea maendeleo ya kiuchumi ndani ya Jumuiya hiyo wilayani Mpanda.

Akihitimisha kikao kazi hicho cha kwanza kwa mwaka 2026, Ndg. Jimotoli Jilala Maduka amewapongeza makatibu kwa mahudhurio mazuri, anawahamasisha kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kuzingatia misingi ya uongozi bora ili kuleta tija katika Jumuiya na Chama cha Mapinduzi.

Kwa pamoja, wajumbe wa kikao wamekubaliana kuyatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa kwa lengo la kuimarisha Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda na kuchangia maendeleo ya chama na jamii kwa ujumla.


Post a Comment

Previous Post Next Post