Waziri wa Madini na Mbunge wa Jimbo la Mtumba, Anthony Mavunde, amesema ana mpango wa kujenga eneo maalumu litakalofanya kazi kama kijiji cha wanawake kwa ajili ya kuwakutanisha wanawake wafanyabiashara katika sehemu moja ili waweze kuuza bidhaa zao kwa pamoja.
Mavunde ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Januari 12, 2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na wanawake kwenye hafla ya kukabidhi vitendea kazi kwa wanawake waliohitimu mafunzo ya ufundi stadi kupitia Chuo cha Veta, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Amesema kijiji hicho kitatoa fursa kwa wanawake kufanya biashara katika mazingira rafiki, kubadilishana uzoefu pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa zao, hali itakayosaidia kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya familia na taifa kwa ujumla.
“Lengo letu ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kwa vitendo, ndiyo maana tunapanga kuwa na eneo maalumu litakalowaunganisha wanawake wote wanaojishughulisha na biashara mbalimbali,” amesema Mavunde.
Aidha, amewataka wanawake wa Jiji la Dodoma kuchangamkia fursa mbalimbali zinazojitokeza ikiwemo mafunzo ya ufundi, mikopo na miradi ya maendeleo ili kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Kwa upande wao, wanufaika wa mafunzo hayo wamesema vitendea kazi walivyokabidhiwa vitawawezesha kuanza na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi, huku wakimshukuru Mavunde na Serikali kwa kuwapa mafunzo na msaada unaowawezesha kujitegemea.
“Tunashukuru kwa mafunzo na vitendea kazi hivi, sasa tuna uhakika wa kuanza kujipatia kipato na kusaidia familia zetu,” amesema Boke Ramadhan
Naye Sylvia Mpanda amesema kuwa wangetamani eneo watakalojengewa basi liwe la mjini ili wawapate wateja wengi kutoka maeneo mbalimbali kwani wateja wengi wanapatikana maeneo yenye watu wengi
"Sisi tutafanya kazi kwa kikundi hivyo kwenye hichi kijiji atakachoanzisha Mhe Mavunde kitakuwa na wanawake wengi hivyo niwatake wanawake wengine kuacha kulala majumbani na waje kuchangamkia fursa zinazotolewa na serikali yetu." Amesema Sylvia
Post a Comment