" MBUNGE BITEGEKO AKAGUA MRADI WA KAHAWA WA VIJANA MAKONGORA, ATOA MILIONI 0.5 KUIMARISHA UTEKELEZAJI, ASISITIZA AJIRA NA UCHUMI KUPITIA KAHAWA ‎

MBUNGE BITEGEKO AKAGUA MRADI WA KAHAWA WA VIJANA MAKONGORA, ATOA MILIONI 0.5 KUIMARISHA UTEKELEZAJI, ASISITIZA AJIRA NA UCHUMI KUPITIA KAHAWA ‎



Na Fabius Clavery, Misalaba Media -Kagera.

Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini, Mhe. Adonis Alfred Bitegeko, akiongozana na viongozi wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Muleba, Januari 4 2025 ametembelea Mradi wa Mashamba Makubwa ya Kahawa uliopo Kijiji cha Makongora, Kata ya Ruhanga, kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wake.

‎Mradi huo unalenga kuwawezesha vijana kiuchumi, kuongeza ajira, kukuza kipato cha wananchi na kuchangia pato la Mkoa wa Kagera, ambapo vijana wananufaika kupitia Programu ya BBT – Jenga Kesho Iliyo Bora.

‎Katika mradi huo, wakulima  wamekabidhiwa jumla ya ekari 300, ambapo zoezi la upandaji wa miche ya kahawa tayari limekamilika, na kwa sasa shughuli za utunzaji wa mashamba zinaendelea chini ya usimamizi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.

‎Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo, Mhe. Bitegeko amesema lengo la ziara hiyo ni kujionea maendeleo ya mradi, kusikiliza changamoto za wakulima, pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha mradi unakuwa endelevu na wenye tija kwa muda mrefu.

‎Amepongeza juhudi za wakulima na vijana wanaoshiriki katika mradi huo, na kuahidi kushirikiana kwa karibu na Kamati ya Siasa Wilaya pamoja na Halmashauri ili kutatua changamoto zitakazojitokeza.

‎Katika kuunga mkono jitihada za vijana, Mhe. Bitegeko amechangia kiasi cha shilingi 500,000/-, kwa ajili ya mfuko wa kusaidiana gharama za matumizi binafsi, huku akiwahimiza wakulima kuzingatia masharti ya mkataba, kufanya kazi kwa bidii na kulinda mradi huo kama mali yao.

‎Ikumbukwe kuwa mradi huu wa vijana umeanzishwa kwa ushirikiano wa karibu na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Hajjath Fatma Mwassa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuwawezesha vijana kiuchumi na kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa mkoani Kagera.



 



Post a Comment

Previous Post Next Post