" MBUNGE BUKOBA MJINI ATOA MAELEKEZO MAKALI KWA MKANDARASI WA KITUO CHA MAGARI

MBUNGE BUKOBA MJINI ATOA MAELEKEZO MAKALI KWA MKANDARASI WA KITUO CHA MAGARI


Na Fabius Clavery, Misalaba Media-Kagera

‎Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini, Mhe. Johnston Mtasingwa, ametembelea na Kukagua mradi wa ujenzi wa kituo kipya cha mabasi katika jimbo hilo, kwa lengo la kukagua maendeleo ya ujenzi na kujiridhisha na kasi ya utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa wananchi.

‎Akiwa katika ziara hiyo, Mhe. Mtasingwa amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa stendi kwa wakati uliopangwa ili wananchi wa Bukoba Mjini waanze kunufaika na huduma zitakazotolewa kupitia stendi hiyo,Amesisitiza kuwa kuchelewa kwa mradi kutawanyima wananchi fursa ya huduma bora za usafiri na biashara.

‎Mbunge huyo pia amemuagiza mkandarasi kukamilisha miundombinu yote muhimu ndani ya kituo hicho, ikiwemo vyoo, maeneo ya kupumzikia abiria, mifumo ya maji na umeme, pamoja na mazingira rafiki kwa watu wote, ili stendi iwe rahisi na salama kwa abiria na watumiaji wengine.

‎Aidha, Mhe. Mtasingwa amewataka wananchi wa Bukoba Mjini kuendelea kumpa ushirikiano katika kipindi cha miaka mitano, akieleza kuwa ushirikiano huo ni msingi muhimu wa kufanikisha utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na miradi ya maendeleo katika jimbo hilo.

‎“Ushirikiano wa wananchi ni nguzo muhimu katika kufanikisha maendeleo. Naomba tuendelee kushirikiana ili kutimiza ahadi tulizozitoa kupitia Ilani ya CCM,” amesema Mhe. Mtasingwa.

‎Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za mbunge huyo kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha inawanufaisha wananchi kama ilivyokusudiwa.




Post a Comment

Previous Post Next Post