" MILIONI 490,652,460 ZAWAKOMBOA WANCHI MANISPAA YA SHINYANGA NA MIKOPO KAUSHA DAMU.

MILIONI 490,652,460 ZAWAKOMBOA WANCHI MANISPAA YA SHINYANGA NA MIKOPO KAUSHA DAMU.

                          Na. Elias Gamaya - Shinyanga

Katika kipindi ambacho wananchi wengi wamejikuta wakinasa katika mtego wa mikopo kandamizi maarufu kama kausha damu, Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda na kuwawezesha wananchi kiuchumi. 

Kupitia mikopo isiyo na riba inayotokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri, zaidi ya shilingi milioni 490 zimekabidhiwa kwa vikundi 30 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika Manispaa ya Shinyanga. 

Hatua hii si tu imefungua fursa mpya za kiuchumi, bali pia imekuwa mwanga wa matumaini kwa wananchi waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za kukosa mitaji na kuingia kwenye mikopo kandamizi.

Hatua hii imedhihirika pale Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, alipokabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya hilingi 490,652,460 kwa vikundi 30 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka Manispaa ya Shinyanga. 

Mikopo hiyo ni sehemu ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri, inayotolewa kwa mujibu wa sera na miongozo ya Serikali kwa lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mhe. Mboni Mhita amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mkazo mkubwa katika uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ili kupunguza umasikini na kuongeza ustawi wa jamii. 

Amesema mikopo hiyo isiyo na riba inalenga kuwainua wananchi wanyonge, kuwapa mitaji ya kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi, sambamba na kuwaepusha kuingia kwenye mikopo kandamizi maarufu kama kausha damu.

“Serikali imeamua kuwashika mkono wananchi wake kwa vitendo. Mikopo hii ni salama, haina riba na inalenga kuhakikisha wananchi wanajikwamua kiuchumi bila kunyonywa,” amesema Mhe. Mboni.

Ameongeza kuwa utoaji wa mikopo hiyo ni ushahidi wa namna Serikali inavyosikiliza na kutatua changamoto za wananchi, huku akisisitiza umuhimu wa wanufaika kusimamia vyema mikopo hiyo ili ilete matokeo chanya kwao binafsi na kwa jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga ambaye pia ni Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Ndg. Peres Kamugisha, amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026 Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imetenga jumla ya Shilingi milioni 800 kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Amefafanua kuwa katika awamu hii, vikundi 30 vilivyokidhi vigezo vimenufaika, ambapo vikundi 20 vya wanawake vimepatiwa jumla ya Shilingi milioni 318, vikundi 9 vya vijana vimepatiwa Shilingi milioni 170.6, huku kikundi kimoja cha watu wenye ulemavu kikipewa Shilingi milioni 2. Amesema mchakato wa utoaji wa mikopo umezingatia uwazi, usawa na vigezo vilivyowekwa na Serikali.

Ndg. Kamugisha ameongeza kuwa kabla ya kupokea mikopo hiyo, vikundi vilipatiwa mafunzo ya uendeshaji wa miradi, usimamizi wa fedha na urejeshaji wa mikopo ili kuhakikisha fedha hizo zinaleta tija na kuleta maendeleo endelevu kwa wanufaika.

Kwa niaba ya vikundi vilivyonufaika, Ndg. Richard John na Ndg. Mussa Nkuba wameishukuru Serikali kwa kuendelea kubuni na kutekeleza mipango ya kuwawezesha wananchi kiuchumi. Wamesema mikopo hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wengi waliokuwa wanategemea mikopo isiyo rasmi yenye riba kubwa na masharti magumu.

“Kwa mikopo hii ya Serikali, tumeepuka kuingia kwenye kausha damu. Tayari tumeshuhudia vijana wengi wakipata ajira kupitia miradi tuliyoanzisha,” wamesema.

Kwa ujumla, utoaji wa mikopo hiyo umeonekana kuwa suluhisho la moja kwa moja kwa changamoto ya mikopo kandamizi, huku ukichochea ujasiriamali, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa wananchi wa Manispaa ya Shinyanga. Hatua hii inaendelea kuonesha dhamira ya dhati ya Serikali katika kujenga uchumi shirikishi unaomjali mwananchi wa kawaida.




Post a Comment

Previous Post Next Post