" MWASELELA AKABIDHI VITI MEZA 200 NA VITI VYAKE SHULE YA SEKONDARI MALAMA, ASEMA ANATEKELEZA SIASA ZA MATENDO

MWASELELA AKABIDHI VITI MEZA 200 NA VITI VYAKE SHULE YA SEKONDARI MALAMA, ASEMA ANATEKELEZA SIASA ZA MATENDO


Na Lydia Lugakila –Misalaba Media

Mbeya

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Mkoa wa Mbeya, Ndele Jailos Mwaselela, amekabidhi jumla ya meza 200 na viti vyake kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Wakili Beno Malisa, kwa ajili ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Malama, iliyopo Mji Mdogo wa Mbalizi, Kata ya Nsalala.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Januari 16,2026 ambapo Mwaselela amesema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira yake ya kuunga mkono maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kufanya siasa za maendeleo na za matendo zinazogusa maisha ya wananchi, hususan wanyonge.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwaselela amesema kiu yake kubwa ni kuhakikisha changamoto ndogo ndogo zinazokwamisha maendeleo ya elimu zinapatiwa ufumbuzi, akisisitiza kuwa siasa zake zimejikita katika kuwaletea wananchi nafuu ya maisha.

“Katika siasa yangu nataka kuwagusa wananchi ili nao wapumue hivyo niwaombe viongozi wenzangu tuendelee kujitoa zaidi katika masuala ya kimaendeleo,” alisema Mwaselela.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Wakili Beno Malisa, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali wananchi wanyonge kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu. 

Aidha, amempongeza Mwaselela kwa kuonesha vitendo katika kutatua changamoto za elimu kwa wanafunzi wa Nsalala na Mkoa wa Mbeya kwa ujumla.

Mhe. Malisa amewahimiza wanafunzi wa Shule ya Sekondari Malama kutunza vifaa hivyo, akisema hatua ya Mwaselela ni kielelezo cha utekelezaji wa majukumu ya chama ndani ya jamii. 

Mkuu wa Mkoa huo Pia amewataka viongozi wengine kuacha kuisubiri Serikali pekee na badala yake kujitoa kwa vitendo katika kuboresha miundombinu ya elimu.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Malama, Bi. Neema Mwakimenye, akisoma taarifa ya shule hiyo, amesema shule ina jumla ya wanafunzi 1,589 na ilikuwa na upungufu wa viti na meza 673, hali iliyokuwa ikiathiri mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Mwakimenye,ameeleza  kuwa mchango wa Mwaselela umefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto hiyo.

Kwa upande wake, Mwaselela amewaahidi walimu, wanafunzi na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mbeya kuwa ataendelea kushirikiana nao na kuhakikisha changamoto ya upungufu wa samani za shule hiyo inamalizika kabisa ndani ya mwaka 2026.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post