Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Licha ya kuongezeka kwa ufaulu wa jumla wa mitihani ya taifa, masomo ya msingi hususan Hisabati (Basic Mathematics) na baadhi ya masomo ya Sayansi yameendelea kuonyesha kushuka kwa viwango vya ufaulu, hali inayozua wasiwasi kuhusu ubora wa elimu nchini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Profesa Said A. Mohamed, wakati akitangaza matokeo ya mitihani ya taifa ya mwaka 2024 na 2025.
Prof. Mohamed amesema ufaulu wa jumla kitaifa umeongezeka kutoka asilimia 32.59 mwaka 2024 hadi asilimia 44.21 mwaka 2025, hatua inayodhihirisha juhudi zinazofanywa katika sekta ya elimu. Hata hivyo, amebainisha kuwa changamoto kubwa bado ipo katika masomo yanayohitaji uelewa wa kina na mazoezi ya mara kwa mara.
Kwa mujibu wa NECTA, somo la Hesabu limeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa wanafunzi wengi, ambapo idadi kubwa ya watahiniwa wamepata madaraja D na F, hali inayohatarisha maendeleo yao katika masomo mengine ya sayansi, teknolojia na fani za kitaalamu.
“Hisabati ni somo la msingi. Kushuka kwa viwango vyake kunaathiri moja kwa moja ufaulu wa masomo ya sayansi na mwelekeo wa wanafunzi katika taaluma za teknolojia na ubunifu,” amesema Prof. Mohamed.
Ameongeza kuwa hali kama hiyo imeonekana pia katika somo la Biolojia, ambapo ufaulu wa madaraja ya juu bado ni mdogo kwa sehemu ya watahiniwa, jambo linaloashiria changamoto katika mbinu za ufundishaji na maandalizi ya wanafunzi.
Hata hivyo, Prof. Mohamed amesema kuna mwanga chanya katika masomo ya ufundi na teknolojia, ambayo yameonyesha kiwango kizuri cha ufaulu kufikia asilimia 81.22, hatua inayothibitisha umuhimu wa elimu ya vitendo katika kuwaandaa vijana kwa soko la ajira.
Akieleza sababu za kushuka kwa viwango katika masomo ya Hisabati na Sayansi, Katibu Mtendaji huyo wa NECTA ametaja uhaba wa walimu wenye umahiri, mtazamo hasi wa wanafunzi kwa masomo magumu, pamoja na ukosefu wa mazoezi ya kutosha darasani.
Kutokana na hali hiyo, Prof. Mohamed ametoa wito kwa wizara husika, walimu, wazazi na wadau wa elimu kuongeza juhudi katika kuboresha mazingira na mbinu za ufundishaji, hususan kwa masomo ya msingi.
“Matokeo haya yanapaswa kuwa funzo na chachu ya mageuzi katika ufundishaji wa Hisabati na Sayansi, ili ufaulu uendane na ubora wa elimu tunayokusudia kuijenga,” amesema
MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE 2025
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment