" PANIKI YA MAREKANI: WACHAMBUZI WAONYA KUHUSU "DEMOKRASIA YA MTUTU" NA UPORAJI WA RASILIMALI

PANIKI YA MAREKANI: WACHAMBUZI WAONYA KUHUSU "DEMOKRASIA YA MTUTU" NA UPORAJI WA RASILIMALI

Rais wa Marekani Donald Trump

Wachambuzi wa masuala ya kistratejia na usalama wameitahadharisha Serikali na mataifa ya Afrika kuwa macho dhidi ya mbinu mpya za Marekani zinazolenga kudhibiti mataifa huru kupitia kile kinachoitwa "demokrasia ya mtutu". 

Onyo hilo limekuja wakati kukiwa na mfululizo wa matukio yanayoashiria kurejea kwa sera za kibeberu zinazotumia nguvu kulinda maslahi ya kiuchumi ya nchi hiyo.

Akizungumza katika kipindi cha ‘Mizani’ cha TBC1 Januari 8, 2026, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia amebainisha kuwa Marekani imekuwa ikitumia ubabe wa kijeshi (Gun Boat Democracy) kinyume na sheria za kimataifa kulinda rasilimali zake. 

Simbakalia alitolea mfano wa nchi ya Venezuela, akieleza kuwa huko nyuma kuliwahi kutokea jaribio la kumteka aliyekuwa Rais Hugo Chavez kabla ya kuokolewa na makomandoo wa nchi hiyo, akisisitiza kuwa mbinu hizo sasa zinaelekezwa maeneo mengine duniani.

Utafiti wa kihistoria unaonyesha kuwa tangu miaka ya 1940, Marekani imehusika katika zaidi ya matukio 80 ya uingiliaji kati, hujuma, na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya mataifa huru. Orodha hiyo inajumuisha nchi kama China (1945), Iran (1953), Vietnam (1961), na Libya (2011) ambapo baada ya uvamizi, nchi hizo ziliachwa katika hali ya machafuko.

Wachambuzi wanaeleza kuwa Marekani hufuata mkondo maalum wa "Kusafisha Ushahidi" kwa kuanza na tuhuma za uongo kupitia vyombo vya habari, kama ilivyokuwa silaha za maangamizi (WMDs) nchini Iraq, kisha hufanya mashambulizi au kuandaa mapinduzi ya serikali na akishapata anachotaka huliacha taifa husika likisambaratika.

Wachambuzi mbalimbali wanasema kwamba vurugu za Marekanio ni matokeo ya kupaniki kwake kuhusiana na masuala ya uchumi na raslimali. Kuinukia kwa mataifa ya China na India kiuchumi kumeanza kuwarejesha katika mazingira ya kuwa mboga na kuendelea kutekeleza mkakati wa Monroe wa kwamba anayetishia usalama wa maslahi ya nchi hiyo utaondolewa kwa nguvu. 

Kwa mujibu wa Kanali Mstaafu Simbakalia, tangu mwaka 1948, Marekani iliyokuwa na asilimia 3 tu ya watu duniani ilidhibiti asilimia 50 ya uchumi wa dunia, na sasa inatumia kila mbinu kuzuia kupoteza utawala huo.

Mhadhiri wa Chuo cha Mipango Dodoma, Dkt. Immaculate Gillo, amesisitiza kuwa mataifa ya Afrika yanapaswa kuimarisha jumuiya za kikanda ili kutengeneza nguvu ya pamoja ya maamuzi. Amesema kuwa umoja huo ndio utakaosaidia kulinda maslahi na rasilimali za bara hili dhidi ya sheria na maelekezo ya kigeni ambayo hayapendi kuona Afrika ikimiliki mali asili zake.

Wachambuzi wamehitimisha kwa kusema kuwa "demokrasia" inayohubiriwa mara nyingi ni janja tu ya kufunika maslahi ya muda mrefu, na kutoa mfano wa taifa la China liliotengeneza mifumo inayolinda watu wao kwanza.


Post a Comment

Previous Post Next Post