……..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa mamlaka za upimaji ardhi na upangaji miji nchini kote zinapaswa kuhakikisha kuwa katika upimaji wa maeneo mapya wanazingatia kutenga maeneo ya kijani pamoja na nafasi ya upandaji miti katika mipango ya makazi na matumizi ya ardhi, ili kuwawezesha wananchi kupanda miti na kujenga makazi yenye ustahimilivu wa kimazingira.
Rais Samia ameyasema hayo tarehe 27 Januari, 2026 katika eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja, mara baada ya kuongoza zoezi la upandaji miti na kuzungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi, wakati wa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa.
Aidha amebainisha kuwa ni muhimu kwa wananchi kujenga utamaduni wa kulinda na kuhifadhi mazingira na kurithisha utamaduni huo kwa watoto, akisisitiza kuwa mtoto anayepanda mti na kuusimamia akiwa mdogo hukua akiwa na upendo kwa mazingira na fikra za kulinda maliasili za nchi.
Amesema kuwa kwa nchi ya Tanzania, athari za uharibifu wa mazingira zinagusa moja kwa moja maisha ya wananchi na ustawi wa Taifa kwa ujumla, ikiwemo changamoto ya kukosekana kwa maji safi na salama, kupungua kwa uzalishaji wa chakula pamoja na kuathiri afya ya mwanadamu.
Aidha amebainisha kuwa upandaji wa miti ni mojawapo ya njia mahsusi za kukabiliana na athari hizo, akieleza kuwa mti unaopandwa na kutunzwa leo utachangia upatikanaji wa mvua siku zijazo, kuifanya ardhi kuwa salama kwa uzalishaji wa chakula, kuhifadhi vyanzo vya maji na kuhakikisha nchi inakuwa na maji ya kutosha kwa ustawi wa wananchi na vizazi vijavyo.
Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizaliwa tarehe 27 Januari, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Post a Comment