" RAIS SAMIA ALIVYOPANDA MITI LEO ZANZIBAR IKIWA NI SEHEMU YA KUMBUKIZI YA KUZALIWA KWAKE

RAIS SAMIA ALIVYOPANDA MITI LEO ZANZIBAR IKIWA NI SEHEMU YA KUMBUKIZI YA KUZALIWA KWAKE






Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikata Keki mara baada ya kuongoza Zoezi la kupanda miti kwenye eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 27 Januari, 2026, wakati wa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa.

Rais Mhe. Dkt. Samia alizaliwa tarehe 27 Januari, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimlisha Keki Mwanafunzi wa Darasa la 6 wa Skuli ya Bungi, Raiyan Ridhiwani mara baada ya kuongoza Zoezi la kupanda miti kwenye eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 27 Januari, 2026, wakati wa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa. Rais Mhe. Dkt. Samia alizaliwa tarehe 27 Januari, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akimlisha Keki Mwanafunzi wa Darasa la 7 wa Skuli ya Bungi, Abdulbasiti Issa mara baada ya kuongoza Zoezi la kupanda miti kwenye eneo la Bungi Kilimo, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe 27 Januari, 2026, wakati wa kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa. Rais Mhe. Dkt. Samia alizaliwa tarehe 27 Januari, 1960 katika Kijiji cha Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.

…………..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameongoza zoezi la upandaji miti katika maeneo ya Bungi Kilimo na Kizimkazi, Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa sambamba na utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji miti ya “27 ya Kijani.”

Akizungumza katika zoezi hilo, Rais Dkt. Samia alisema ameichagua siku yake ya kuzaliwa kuwa siku ya kupanda miti kama ishara ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu, pamoja na kutimiza wajibu wake wa kulinda mazingira na kuacha urithi endelevu kwa vizazi vijavyo. Alisisitiza kuwa jukumu la kulinda mazingira ni la kila Mtanzania kupitia upandaji na utunzaji wa miti ili kurejesha uoto wa asili uliopotea.

Rais Samia alieleza kuwa Tanzania inakabiliwa na ongezeko la idadi ya watu linalokaribia kufikia milioni 70, hali inayohitaji jitihada za pamoja katika kulinda mazingira. Alisema endapo Watanzania milioni 30 kila mmoja atapanda na kutunza angalau mti mmoja kila mwaka, taifa litakuwa limechukua hatua muhimu kuelekea ulinzi na mustakabali endelevu wa mazingira.

Aidha, Rais alibainisha kuwa mabadiliko ya tabianchi ni uhalisia unaoathiri maisha ya wananchi kupitia ukame, mvua zisizotabirika, mafuriko, ongezeko la joto na kuongezeka kwa kina cha bahari. Alisisitiza kuwa upandaji na utunzaji wa miti ni miongoni mwa suluhisho mahsusi ya kukabiliana na athari hizo kwa kuhifadhi vyanzo vya maji, kuimarisha uzalishaji wa chakula, kuboresha afya ya binadamu na kulinda bioanuwai.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia alisisitiza umuhimu wa kuwahusisha watoto katika juhudi za utunzaji wa mazingira, akieleza kuwa malezi ya mapema hujenga kizazi chenye uelewa na uwajibikaji wa kulinda maliasili za taifa.

“Mtoto akipanda mti na akausimamia akiwa mdogo, anakua akiwa na upendo wa mazingira na fikra za kulinda maliasili za nchi yetu,” alisema Rais Samia.

Akieleza malengo ya zoezi hilo, Rais Samia alisema upandaji miti ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya kitaifa ya kukuza sekta ya kilimo na kuongeza mchango wake katika pato la taifa, sambamba na fursa za kiuchumi zitokanazo na biashara ya hewa ukaa kupitia misitu inayolindwa na kurejeshwa.

Kimataifa, Rais Samia alisema Tanzania inaendelea kuunga mkono kwa vitendo Ajenda ya Maendeleo Endelevu 2030, hususan malengo ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kulinda uhai katika ardhi, kuhakikisha usalama wa chakula, afya ya jamii na upatikanaji wa maji safi.

Katika hotuba yake, Rais aliwashukuru Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kuanzisha na kuendeleza kampeni ya “27 ya Kijani,” pamoja na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFSA) na wadau wengine kwa kusimamia, kuhamasisha na kuwezesha upandaji wa miti nchini kote.

Kampeni ya kitaifa ya “27 ya Kijani” ilianzishwa mwaka 2023. Tangu kuanza kwake, jumla ya miche ya miti 113,199,359 ya aina mbalimbali imekuzwa na kupandwa nchini kote. Kati ya hiyo, miche 46,488,315 imetolewa kwa wananchi kwa ajili ya upandaji katika maeneo yao, huku miche 66,711,044 ikipandwa katika hifadhi za misitu na mashamba ya miti.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post