Serikali imetoa onyo kali dhidi ya kundi la watu wanaotumia vibaya teknolojia kwa kukata na kusambaza vipande vya video (clips) kwenye mitandao ya kijamii, vikiwa na lengo la kupotosha umma na kuchochea mipasuko ya kikabila, kikanda, na kisiasa nchini.
Tahadhari hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, mjini Dodoma, alipokuwa akizungumza na menejimenti ya wizara yake. Waziri Katambi amebainisha kuwa utamaduni wa kuhariri maudhui ili kuleta picha potofu ni "nia ovu" kisheria na ni uhujumu wa amani iliyoasisiwa na waasisi wa taifa hili.
Kitendo hicho cha kukata video kinafananishwa na kuchochea balaa na kwamba serikali haitavumilia. Aidha serikali imewaambia Watanzania kwa kauli yake kwamba kuchochea balaa si namna bora ya kuwa binadamu na kutaka wananchi kuona umuhimu wa kila mtumiaji wa mitandao ya kijamii kujiridhisha na ukweli wa taarifa kabla ya kuisambaza.
Kutengeneza video za uchochezi kunaweza kuonekana kama mchezo wa kupata "views" au "likes," za kutosha lakini gharama yake ni kupoteza utulivu ambao Tanzania imejivunia kwa miongo sita.
Waziri Katambi amefafanua kuwa kuna watu wamebobea katika kukata video za viongozi au wananchi na kuziacha bila muktadha (context), jambo linalosababisha taharuki na kudhalilisha wahusika. Mbinu hizi zinatajwa kutumika kama ajenda ya kusukuma mipasuko ya kijamii na kudhoofisha umoja wa kitaifa.
"Kugawanya viongozi kwa kutumia vipande vya video ambavyo havijazingatia usawa wa pande zote ni kitendo cha kudhalilisha na kutweza utu. Tafsiri yake ni kwamba aliyekata kipande hicho ana nia ovu ya kuleta taharuki," alisema Waziri Katambi.
Ameongeza kuwa Serikali haitasita kuwaita wahusika wa vitendo hivyo ili watoe maelezo ya kina kuhusu dhamira yao ya kutaka kuligawa taifa. Lengo ni kupima faida wanayoiona wao dhidi ya hasara kubwa ambayo taifa linaweza kuipata kupitia uvunjifu wa amani.
Pamoja na onyo hilo, Waziri Katambi amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaongozwa na falsafa ya kutafuta suluhu (R4). Alibainisha kuwa milango iko wazi kwa majadiliano ya kisheria na pale itakapobainika mtu yuko sahihi, haki yake itatolewa bila upendeleo.
"Mimi niko tayari kuzungumza na Watanzania na kuwaeleza ukweli. Sehemu tutakayoona mtu yuko sahihi, haki yake ataipata. Huo ndiyo msingi wa Rais Samia, mama anayetafuta suluhu na ndiyo maana ameunda hata tume mbalimbali," alisisitiza Katambi.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohamed Mahmoud, amewataka watumishi wa wizara hiyo kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu ili kufikia matarajio ya Rais na Watanzania. Alisema kuwa maelekezo yaliyotolewa na Waziri Katambi ndiyo yatakuwa dira ya wizara katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unalindwa kwa kuzingatia haki.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment