" SERIKALI YATENGA DOLA MILIONI 12 KUPUNGUZA VIFO VYA AKINAMAMA NA WATOTO

SERIKALI YATENGA DOLA MILIONI 12 KUPUNGUZA VIFO VYA AKINAMAMA NA WATOTO






Mkurugenzi wa huduma za mama na mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ahmed Makuani akizungumza kwenye uzinduzi wa kupunguza vifo vya akinamama na watoto leo Januari 29, 2026 Jijini Dodoma. Wataalam wa afya waliohudhuria uzinduzi wa program ya kupunguza vifo vya akinamama na watoto wakati wa kujifungua Jijini Dodoma. Programu hiyo inaendeshwa na Shirika lisilo la kiserikali la Thamini Uhai.

Na Meleka Kulwa – Fullshangwe Blog, Dodoma

Serikali kwa kushirikiana na wadau wa afya imeanzisha programu maalum ya miaka mitano yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 12, inayolenga kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto chini ya miaka mitano katika mikoa ya Geita, Katavi na Kigoma kuanzia mwaka 2025 hadi 2030.

Programu hiyo inalenga kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto ili kufikia malengo ya kitaifa ya kupunguza vifo hivyo ifikapo mwaka 2030, ambapo vifo vya akinamama vinatarajiwa kufikia 75 kwa vizazi hai 100,000, vifo vya watoto wachanga kufikia 12 kwa vizazi hai 1,000 na watoto chini ya miaka mitano kufikia vifo 25 kwa vizazi hai 1,000.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo Januari 29,2026 jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Huduma za Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ahmed Makuani amesema kuwa bado vifo vitokanavyo na uzazi ni changamoto kubwa, akisisitiza kuwa kifo cha mama mmoja wakati wa kujifungua hakiwezi kuonekana kama takwimu bali ni pigo kwa familia na jamii kwa ujumla.

Amesema kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hiyo, ambapo takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa akina mama 556 walifariki kati ya vizazi hai 100,000, huku hadi mwaka 2022 idadi hiyo ikishuka hadi vifo 104 kwa vizazi hai 100,000 sawa na upungufu wa asilimia 80.

Aidha amebainisha kuwa mkakati wa sasa wa Serikali haujajikita tu kwenye kupunguza vifo, bali pia kuimarisha lishe bora kwa akinamama na watoto ili kuhakikisha wanapata huduma kamili na endelevu.

Dkt. Makuani amesema kuwa licha ya jitihada za kutumia mashine za kuwasaidia watoto kupumua mara baada ya kuzaliwa (HBB), changamoto kubwa bado ipo kwa ufuatiliaji wa watoto hao wanaporejea majumbani kutokana na uhaba wa wataalam wa afya, hali inayosababisha vifo vinavyotokana na magonjwa kama homa, kuharisha na nimonia.

Amesema kuwa nguvu zaidi zinapaswa kuelekezwa katika kuimarisha wodi za watoto wenye umri chini ya miaka mitano ili kupunguza vifo vinavyojitokeza baada ya watoto kuruhusiwa kutoka hospitalini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Thamini Uhai, Banzi Msumi amesema kuwa fedha hizo za Dola za Marekani milioni 12 zimeelekezwa katika uboreshaji wa miundombinu ya afya pamoja na kutoa mafunzo kwa wauguzi, wakunga na watumishi wa afya katika mikoa hiyo mitatu.

Amesema kuwa mradi huo pia umejikita katika kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya muda na wenye uzito mdogo kwa kujenga wodi maalum za kuwahifadhi wakati wakiendelea kupata matibabu, kundi ambalo limeonekana kuchangia kwa kiasi kikubwa vifo vya watoto wachanga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Dina Tinda amesema kuwa ofisi hiyo iko tayari kushirikiana na wadau wote wa maendeleo ili kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa na kusaidia Serikali kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Akiwawakilisha wakuu wa mikoa ya Geita, Katavi na Kigoma, Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Mhe. Majid Mwanga amesema kuwa changamoto za sekta ya afya zitaendelea kujadiliwa katika vikao vya mikoa, wilaya na vikao vya usalama ili kuhakikisha maamuzi yanayochukuliwa yanazingatia uhalisia wa changamoto zilizopo.

Amesema kuwa baadhi ya changamoto za kiafya kwa wanawake wajawazito hupelekea madhara wakati wa kujifungua, lakini kutokana na uelewa mdogo wa masuala ya kitabibu, mara nyingine lawama hupelekwa kwa watumishi wa afya bila uchunguzi wa kina.

Aidha amebainisha kuwa kupitia majadiliano ya pamoja ya changamoto za sekta ya afya, matukio yanapojitokeza yataweza kutatuliwa kwa busara na kwa kuzingatia taratibu sahihi badala ya kuchukua hatua za haraka zisizo na tija.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post