" SHIRIKA LA COWOCE LATOA MAFUNZO YA VICOBA, LALENGA KUINUA UCHUMI WA WANANCHI MANISPAA YA SHINYANGA

SHIRIKA LA COWOCE LATOA MAFUNZO YA VICOBA, LALENGA KUINUA UCHUMI WA WANANCHI MANISPAA YA SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Shirika la Companion of Women and Children Empowerment (COWOCE) limefanya mafunzo maalum kwa vikundi vya VICOBA leo tarehe 17 Januari 2026 katika Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuinua uchumi wa wananchi na kuwawezesha kiuchumi.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Shirika la COWOCE yakilenga kuwajengea uwezo wanachama wa VICOBA katika uendeshaji wa vikundi vyao, usimamizi wa fedha na matumizi sahihi ya mikopo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi ambapo mafunzo hayo yamehudhuriwa na wanachama kutoka vikundi mbalimbali vya VICOBA vilivyopo Manispaa ya Shinyanga.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Shirika la COWOCE, Bwana Joseph Ndatala, amesema lengo kuu la shirika hilo ni kuwawezesha wananchi kiuchumi kwa kuwapa elimu sahihi itakayowasaidia kujitegemea na kuboresha maisha yao ya kila siku.

Kwa upande wake, Meneja wa Shirika la COWOCE, Veronica Kipangule, ameeleza kuwa shirika hilo limejikita katika kusaidia makundi mbalimbali hususan wanawake na vijana kupitia mafunzo ya ujasiriamali, VICOBA pamoja na miradi midogo midogo ya kiuchumi yenye tija kwa familia na jamii kwa ujumla.

Mada ya kwanza imewasilishwa na Mkufunzi wa COWOCE Bwana Joseph Ndatala, ikilenga kuwajengea wanachama uelewa wa dhana ya VICOBA, umuhimu wake na namna ya kuendesha kikundi kwa ufanisi.

Katika mada hiyo, washiriki wamejifunza maana ya VICOBA, malengo na faida zake, kanuni na taratibu za uendeshaji, muundo wa kikundi pamoja na haki na wajibu wa mwanachama. Mafunzo hayo yanatolewa kwa njia ya majadiliano ya pamoja, maswali na majibu pamoja na mifano halisi kutoka katika vikundi vya washiriki.

Imeelezwa kuwa VICOBA ni vikundi vya watu wanaojikusanya kwa hiari ili kuweka akiba, kukopeshana fedha na kusaidiana kiuchumi, huku malengo yake yakiwa ni kukuza tabia ya kujiwekea akiba, kutoa mikopo midogo kwa wanachama, kuimarisha umoja na mshikamano na kuinua kipato cha familia na jamii.

Ndatala ametaja faida za VICOBA kuwa ni urahisi wa kujiunga na kuendesha, kutokuwa na masharti magumu kama ya benki, kutoa mikopo kwa wakati pamoja na kujenga nidhamu ya kifedha kwa wanachama.

Washiriki pia wamejifunza muundo wa VICOBA unaojumuisha Mwenyekiti, Katibu, Mweka Hazina na wajumbe wa kamati, ambapo kila kiongozi anawajibika kusimamia kikundi kwa uaminifu na uwazi.

Mada ya pili imelenga kuwajengea wanachama uwezo wa kusimamia fedha za kikundi na mikopo kwa uwazi na nidhamu ambapo washiriki wamefundishwa kuhusu akiba na michango ya wanachama, utunzaji wa fedha kwa kutumia sanduku lenye funguo tatu au benki, pamoja na umuhimu wa kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi.

Aidha, masharti ya mikopo, riba na marejesho yameelezewa kwa kina, huku mkazo mkubwa ukiwekwa kwenye athari za mikopo chechefu ambayo husababisha kukosekana kwa fedha kwenye kikundi, migogoro miongoni mwa wanachama na kudhoofika kwa VICOBA.

Katika mada hiyo, washiriki wanafanya mazoezi ya vitendo ikiwemo hesabu rahisi za mkopo, mfano wa mkopo wa shilingi 300,000 kwa riba ya asilimia 15, ili kuwajengea uelewa wa vitendo kuhusu marejesho.

Mada ya tatu imelenga kuwasaidia wanachama kutumia mikopo ya VICOBA katika shughuli za kiuchumi zitakazowaongezea kipato. Washiriki wanafundishwa maana ya ujasiriamali, sifa za mjasiriamali bora, uchaguzi wa biashara ndogo, matumizi sahihi ya mkopo pamoja na namna ya kutenganisha fedha za biashara na matumizi ya nyumbani.

Imeelezwa kuwa ujasiriamali ni uwezo wa kuona fursa, kuanzisha au kuboresha shughuli za kiuchumi na kuchukua hatua kwa ujasiri ili kupata faida na kuboresha maisha. Washiriki wanahimizwa kutumia mikopo kwa biashara zenye soko, kuendana na mazingira yao na kuanza kwa mtaji mdogo.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwemo akina mama wanufaika wa miradi ya Shirika la COWOCE, wameeleza kuridhishwa na mafunzo hayo wakisema yamewapa uelewa mpana juu ya uendeshaji sahihi wa VICOBA, usimamizi wa fedha na matumizi bora ya mikopo.

Wanufaika hao wanaeleza kuwa kabla ya mafunzo walikuwa wakikumbana na changamoto mbalimbali ikiwemo mikopo chechefu, migogoro ndani ya vikundi pamoja na matumizi yasiyo sahihi ya fedha za mikopo.

Akina mama hao wameeleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kuimarisha vikundi vyao, kuongeza nidhamu ya kifedha, kukuza biashara ndogo ndogo wanazozifanya pamoja na kuboresha maisha ya familia zao huku akilishukuru shirika la COWOCE kwa kuendelea kuwa karibu na jamii kwa vitendo kupitia mafunzo, miradi ya kiuchumi na misaada ya kijamii ikiwemo elimu na mradi wa nguruwe unaolenga ustawi wa watoto.

Wanufaika hao wameahidi kutumia maarifa waliyoyapata kuleta mabadiliko chanya katika vikundi vyao na kuwa mabalozi wa VICOBA bora katika jamii zao, huku wakiiomba COWOCE kuendelea kutoa mafunzo ya mara kwa mara ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wa Mkoa wa Shinyanga.

Katika hatua nyingine, Shirika la COWOCE limekabidhi msaada wa madaftari kwa wanafunzi wa shule za msingi zilizopo Kata ya Ndala, ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika kuboresha mazingira ya elimu.

Vilevile, shirika hilo lina utaratibu wa utekelezaji wa mradi wa nguruwe, ambapo hugawa nguruwe wawili kwa kila familia, nguruwe hao wakilenga kusaidia mahitaji ya watoto ikiwemo kugharamia masomo yao, hatua inayolenga kusaidia watoto kutimiza ndoto zao za kielimu.

Mkurugenzi wa Shirika la COWOCE, Bwana Joseph Ndatala, akizungumza na washiriki wakati wa mafunzo ya VICOBA yaliyofanyika leo tarehe 17 Januari 2026 mjini Shinyanga.




   

Post a Comment

Previous Post Next Post