Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF) imetangaza kuandaa mkutano maalumu wa mazungumzo ya kitaifa kuhusu Amani, Umoja, Haki na Maendeleo ya Tanzania, utakaofanyika Januari 22, 2026 katika Ukumbi wa Mikutano wa Taasisi hiyo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Taasisi hiyo, Joseph Waryoba Butiku, amesema mkutano huo umelenga kutoa jukwaa kwa wazee wenye busara na hekima kujadili misingi ya taifa iliyoasisiwa na waasisi wake, hususan Mwalimu Julius Nyerere, iliyowezesha Tanzania kudumisha amani na mshikamano kwa miongo kadhaa.
Butiku amesema falsafa ya kumshirikisha “mzee” haijiegemezi katika vyeo au hadhi, bali hekima na uzoefu wa maisha. “Mwalimu aliamini sana katika nafasi ya wazee. Hata kama ni Askofu, akiwa hapa anakuja kama mzee, si kwa cheo chake,” amesema.
Ameeleza kuwa mkutano huo utawakutanisha wazee kwa tafsiri pana, wakiwemo viongozi wa dini, wasomi, wastaafu, wanawake, vijana, wanasiasa, wadau wa sekta ya habari pamoja na taasisi za kiraia, kwa lengo la kutafakari mustakabali wa taifa.
Kwa mujibu wa Butiku, uamuzi wa kuandaa mazungumzo hayo umetokana na matukio ya ghasia na kuvurugika kwa amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani uliofanyika Oktoba 29, 2025.
“Tulichokiona Oktoba 29 kilitupa maswali mengi. Vijana walihusishwa katika mapambano na vyombo vya dola, wananchi wakaambiwa wakae ndani, lakini sauti za viongozi wa kisiasa hazikusikika,” amesema.
Amebainisha kuwa hali hiyo ilionesha kuyumba kwa misingi ya utawala wa sheria na kuliacha taifa katika huzuni na sintofahamu, jambo lililopelekea Rais kuunda Tume ya Uchunguzi kuchunguza yaliyojiri.
Butiku ameongeza kuwa Rais pia alielekeza kuanzishwa kwa jukwaa la uzalendo na maadili, litakalosaidia kurejesha na kuimarisha misingi ya taifa kwa kuenzi maono ya Mwalimu Nyerere, ikiwemo kulinda amani na usalama, kukuza maadili na utaifa, kujitegemea, pamoja na kuhimiza maendeleo ya kiuchumi hususan kupitia sekta ya kilimo.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment