" TANFORD KUNADI TANZANIA KIMATAIFA KUPITIA KONGAMANO LA BIASHARA NA USAFIRISHAJI DUBAI

TANFORD KUNADI TANZANIA KIMATAIFA KUPITIA KONGAMANO LA BIASHARA NA USAFIRISHAJI DUBAI

‎ Chama cha Tanzania Freight Forwarders Representation in Dubai (TANFORD) kimeandaa kongamano la siku mbili litakalofanyika Februari 13 na 14, 2026 Dubai, Umoja wa Nchi za Kiarabu, likiwa na lengo la kuinadi Tanzania katika masoko ya kimataifa ya biashara na usafirishaji.‎Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa TANFORD, Bw. Hussein Jamal, amesema kongamano hilo linaloitwa Tanzania Trade and Logistics Forum 2026 linatarajiwa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya biashara, usafirishaji na uwekezaji kutoka mataifa tofauti, kwa lengo la kufungua na kuimarisha fursa za kiuchumi kati ya Tanzania na Dubai.‎Alisema TANFORD imelenga kulitumia kongamano hilo kuitangaza Tanzania kama kitovu cha biashara na usafirishaji katika Afrika Mashariki na Kati, sambamba na kukuza matumizi ya bandari na miundombinu ya usafirishaji nchini.‎“Lengo letu ni kuifanya Tanzania kuwa lango la kupitisha mizigo ya kimataifa kwa kutumia bandari zetu, pamoja na kuvutia wafanyabiashara na wawekezaji wa kimataifa kutumia miundombinu ya usafirishaji iliyopo nchini,” amesema Bw. Jamal.‎Ameongeza kuwa kongamano hilo litatoa fursa kwa bidhaa za Tanzania kupata masoko mapya ya kimataifa kupitia mikutano ya moja kwa moja na wanunuzi na wadau wa biashara watakaoshiriki katika kongamano hilo.‎“TANFORD inasimama kama daraja la kibiashara kati ya Tanzania na masoko ya kimataifa kwa kuwasaidia wafanyabiashara wa Kitanzania kutambua na kunufaika na fursa zilizopo Dubai, sambamba na kutangaza biashara zao kimataifa,” amesema.‎Bw. Jamal amebainisha kuwa TANFORD pia inaunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza matumizi ya bandari na miundombinu ya usafirishaji kwa kuunganisha mizigo ya masoko ya kimataifa inayopita katika bandari za Tanzania.‎Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TanTrade, Dkt. Latifa Mohammed Khamis, amesema ushiriki katika makongamano ya kimataifa ni muhimu kwa wafanyabiashara wa Kitanzania kwani husaidia kuimarisha mahusiano ya kibiashara na washirika wa nje ya nchi.‎“Ni muhimu wafanyabiashara wa Kitanzania kushiriki katika kongamano hili kwani litatoa fursa ya kupata ushirikiano mpya wa kibiashara na wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali,” amesema Dkt. Latifa.‎Naye Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Bw. Edwin Urio, amesema kongamano hilo ni fursa muhimu kwa wadau wa sekta ya usafirishaji kujitangaza, kujikuza kibiashara na kuchangia kukuza uchumi wa taifa.‎“Sekta ya usafirishaji na lojistiki ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa lolote. Katika mwaka wa fedha 2024/2025, sekta hii imeongoza kwa kuingiza fedha za kigeni nchini,” amesema Bw. Urio.‎Aidha amezipongeza taasisi za Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi katika maandalizi ya kongamano hilo, akisema lina mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa nchi.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post