" UVAMIZI VENEZUELA NI KITU CHA KUHOJI

UVAMIZI VENEZUELA NI KITU CHA KUHOJI

KATIKA kile kinachoonekana kama mtihani mzito kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN) na uhuru wa mataifa madogo duniani, mtaalamu wa masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa, Christopher Makwaia, amechambua kwa kina anguko la Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro.

Makwaia anabainisha kuwa kukamatwa kwa Maduro na mkewe, Cilia Flores, Januari 3, 2026, kufuatia shambulio la anga la Marekani jijini Caracas, kumeibua maswali magumu kuhusu mustakabali wa sheria za kimataifa dhidi ya mataifa yenye nguvu.

Katika uchambuzi wake, Makwaia anahoji: "Je, sheria za kimataifa ni kinga ya wote, au ni lugha inayozungumzwa tu pale wenye nguvu wanaporuhusu?" Anabainisha kuwa kitendo cha Marekani kuingia katika ardhi ya nchi huru na kumkamata kiongozi aliyeko madarakani ni ukiukwaji wa wazi wa Ibara ya 2(4) ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Licha ya Marekani kudai kuwa ilikuwa ni operesheni ya "kusimamia sheria" kutokana na tuhuma mbalimbali, Makwaia anaonya kuwa hatua hii inatengeneza mfano mbaya ambapo mataifa makubwa yanaweza kuvamia nchi yoyote kwa kisingizio cha kujifanya polisi.

Sehemu muhimu katika makala ya Makwaia ni uhusiano kati ya operesheni hiyo na utajiri wa mafuta wa Venezuela. Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, tamko la Rais Donald Trump kuwa Marekani itasimamia sekta ya mafuta ya nchi hiyo, linathibitisha kuwa rasilimali ndizo kiini cha mgogoro.

"Je, rasilimali za nchi ni mali ya wananchi kwa haki ya uhuru wao, au zinakuwa mali ya yule mwenye nguvu za kijeshi? Mataifa madogo yanaweza kujikuta yakichaguliwa washirika wa kibiashara na mataifa makubwa, na ushirika huo ukageuka kuwa liability (mzigo) pindi maslahi ya wenye nguvu yanapoguswa."

Makwaia katika maandiko yake anaonya  kuwa hakuna cha kushangilia kwa tukio hilo kwani dunia inaingia katika zama ambapo "Mwenye Nguvu ndiye Mwenye Haki." 

Anabainisha kuwa ikiwa Umoja wa Mataifa utashindwa kuzuia vitendo hivi, mataifa madogo yataacha kuamini diplomasia na badala yake kuanza kujiimarisha kijeshi ili kulinda uhuru wao, jambo ambalo litaifanya dunia kuwa mahali hatari zaidi.



Post a Comment

Previous Post Next Post