
Na Meleka Kulwa, Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imefanikiwa kuwasajili wafanyabiashara ndogondogo 119,595 ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita kipindi cha pili, ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya kurasimisha sekta isiyo rasmi nchini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dodoma Januari 25, 2026, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuwa kwa mujibu wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, jumla ya wafanyabiashara ndogondogo 1,175,617 wakitambuliwa.
Amesema kuwa usajili wa wafanyabiashara hao umefanyika kupitia Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Wafanyabiashara Ndogondogo (WBNMIS) kwa lengo la kuwawezesha kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazotolewa na Serikali.
Amesema kuwa kati ya wafanyabiashara waliosajiliwa, wanawake ni 73,341 huku wanaume wakiwa 46,254. Amesema kuwa katika mgawanyo wa makundi, wafanyabiashara wa Machinga ni 103,102, Mama na Baba Lishe ni 12,384 na waendesha Bodaboda na Bajaji ni 4,109.
Aidha amebainisha kuwa pamoja na usajili, Serikali imepokea jumla ya Shilingi bilioni 10.5 kwa ajili ya kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wafanyabiashara ndogondogo, ambapo tayari Shilingi 1,351,660,000.00 zimetolewa kwa wafanyabiashara 588 kupitia Benki ya NMB na zoezi hilo linaendelea nchi nzima.
Amesema kuwa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Shilingi 337,970,000 zimetolewa kwa wanawake wajasiriamali 45 kwa riba ya asilimia nne.
Aidha amebainisha kuwa katika kuimarisha urasimishaji kwa waendesha vyombo vya usafiri, kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), jumla ya waendesha pikipiki na bajaji 209,632 wamerasimishwa kwa kupatiwa leseni za udereva, huku zoezi hilo likiendelea.
Amesema kuwa kupitia mfumo wa Wezesha Portal unaosimamiwa na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, vikundi 6,041 vya wajasiriamali vimetambuliwa na kusajiliwa, vikiwemo vikundi vya wanawake 3,207, vijana 2,318 na watu wenye ulemavu 516, vyenye jumla ya wanufaika 30,205.
Aidha amebainisha kuwa kupitia mfumo wa TAUSI, leseni 125,621 zimetolewa kwa wajasiriamali, hatua iliyowezesha utoaji wa mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri yenye thamani ya Shilingi bilioni 33.45 kwa vikundi 3,776 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Amebainisha kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) imerasimisha wajasiriamali 16,325, ambapo wajasiriamali 11,000 wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali, 12,325 wamepata mikopo na zaidi ya 3,900 wamepatiwa namba za mlipa kodi (TIN) na leseni za biashara.
Aidha amebainisha kuwa kupitia SIDO, mikopo 265 yenye thamani ya Shilingi 1,085,900,000 imetolewa ndani ya kipindi hicho na kuweza kutoa ajira 652, kati ya hizo ajira 489 ni za vijana.
Pia, Amesema kuwa Serikali itaendelea kuhamasisha wafanyabiashara ndogondogo kujitokeza kwa wingi kujisajili kwenye mifumo rasmi ili kunufaika na fursa za kiuchumi chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment