Na Fabius Clavery,Misalaba Media-Kagera.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe limeidhinisha na kupitisha bajeti ya Shilingi bilioni 69.5 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma na kuongeza kasi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Bajeti hiyo imepitishwa Februari 17, 2026, katika kikao maalum cha baraza kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri (Angaza), ambapo madiwani walijadili na kuafikiana juu ya vipaumbele vya utekelezaji kwa mwaka ujao wa fedha.
Baraza limeweka mikakati madhubuti ya kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuhakikisha mianya yote ya upotevu wa mapato inazibwa, pamoja na kuibua na kuendeleza vyanzo vipya vya mapato. Hatua hiyo inalenga kuiwezesha halmashauri kupanua wigo wa bajeti na kuongeza fedha za miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Longino, amesema,
“Tumejipanga kuongeza ukusanyaji wa mapato kwa kuhakikisha tunaziba mianya yote ya upotevu wa mapato. Pia tunaendelea kuibua vyanzo vipya ili kufikia lengo la kupandisha ukomo wa bajeti (budget ceiling) kutoka kiwango cha sasa kwenda kiwango cha juu zaidi. Mapato yakivuka bajeti tuliyoweka, fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya maendeleo ambayo haikupangwa kwenye bajeti ya awali.”
Miongoni mwa vipaumbele vilivyoidhinishwa kutekelezwa katika mwaka wa Fedha 2026/27.Uendelezaji wa miradi yenye kuongeza mapato ya halmashauri,Ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za kata,Upimaji na ulipaji fidia wa maeneo ya taasisi za halmashauri,Uendelezaji na uzalishaji wa miche ya kahawa,Ukamilishaji wa Kituo cha Afya Nyakakika pamoja na Ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule za msingi na sekondari.
Kwa upande wake, Innocent Bashungwa ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Karagwe, amesema atahakikisha anapambania bajeti hiyo katika Bunge la Bajeti ili ipate mafanikio yaliyokusudiwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani akieleza kuwa bila amani wananchi hawawezi kufanya shughuli zao za kiuchumi wala miradi ya maendeleo kutekelezwa kwa ufanisi. Pia aliwataka madiwani kuijadili bajeti hiyo kwa uwazi na ujasiri ili maamuzi yanayopitishwa yaendane na matarajio ya wananchi.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo, katika bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/2027 kunatarajiwa kujengwa soko kubwa la wilaya katika Kata ya Kayanga pamoja na stendi ya mabasi (Kishao), miradi ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2030.
Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatajwa kuwa hatua muhimu katika kuimarisha maendeleo ya Karagwe, huku viongozi wakisisitiza ushirikiano wa wananchi katika kuongeza mapato na kulinda rasilimali za umma.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254










Post a Comment