" KATAMBI ANYOOSHA MAELEZO: "AMANI YETU SI YA MCHEZO," AONYA WANAOCHAFUA NCHI MITANDAONI

KATAMBI ANYOOSHA MAELEZO: "AMANI YETU SI YA MCHEZO," AONYA WANAOCHAFUA NCHI MITANDAONI

Mbunge wa Shinyanga Mjini na Waziri, Patrobas Katambi, ametoa onyo kali kwa watu na makundi yanayotumika kuichafua taswira ya Tanzania kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa amani ya nchi ni tunu isiyopaswa kuchezewa na yeyote kwa maslahi ya kisiasa au chuki.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa kushukuru wananchi wa Shinyanga Mjini kwa kumpa ridhaa ya kuwaongoza, Katambi amewashangaa watu wanaofurahia kusambaza picha na video (picha za mjongeo) zenye viashiria vya uvunjifu wa amani, akibainisha kuwa vitendo hivyo ni hatari kwa usalama wa taifa.

Katambi amesema kuwa amani ikivurugika, kuirejesha ni kazi ngumu na yenye gharama kubwa, hivyo akawataka Watanzania kupuuza kundi linalolenga kutengeneza taharuki ili kuwatoa wananchi kwenye reli ya maendeleo.

"Tanzania itaendelea kuwa na amani na utulivu. Watu wasione raha kuchukua nakala au picha zinazohatarisha usalama na kuzisambaza. Amani ikitoweka, sote tutaumia. Tuishi kwa upendo bila ubaguzi," alisisitiza Katambi.

Aidha, alielekeza rungu lake kwa watumishi wa serikali wazembe, akisema mwisho wao umefika. Alibainisha kuwa serikali inatoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini baadhi ya watumishi wanachelewesha utekelezaji kwa uzembe, jambo ambalo halitafumbiwa macho.

Ili kuonyesha kuwa serikali imejikita kwenye maendeleo na si maneno, Katambi alitangaza kuwa zaidi ya Shilingi bilioni 45 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Ibadakuli mkoani Shinyanga, mradi utakaofungua fursa za kiuchumi na usafiri.

Katika mkutano huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga kamishna mwandamizi wa Polisi, Janeti Magomi, alihakikishia umma kuwa hali ya ulinzi na usalama mkoani humo ni shwari, huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Mabala Mlolwa, akitaka vitambulisho vya Taifa (NIDA) vifikishwe hadi ngazi za kata ili kupunguza usumbufu kwa wananchi.

Wadau mbalimbali wa amani wameungana na Katambi kulaani makundi yanayotaka kuigawa nchi. Mkurugenzi wa African Talent Forum (ATF), Rosemary Bujashi, ameitaja amani kama ngao ya nchi inayopaswa kulindwa kwa gharama yoyote.

"Tuachane na wale wanaotaka kutugawa. Amani ni silaha yetu dhidi ya wasioitakia mema nchi yetu," alisema Bujashi.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani (JMAT) Wilaya ya Mkuranga, Shukuru Ngweshani, pamoja na Diwani wa Kata ya Mkuranga, Hamza Mahanaka, wamewasihi vijana kujiepusha na makundi yanayoyumbisha nchi kiuchumi na badala yake wahubiri upendo ili kuvutia wawekezaji na kudumisha mshikamano wa kitaifa.

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment

Previous Post Next Post