Na Lydia Lugakila-Misalaba Media
Kyerwa
Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa imeandika historia baada ya kuandaa bonanza kubwa la michezo lililowakutanisha watumishi wanamichezo kutoka Halmashauri sita (6) za Mkoa wa Kagera, huku Muleba ikiibuka bingwa wa jumla na Kyerwa kushika nafasi ya pili.
Bonanza hilo, limefanyika Februari 21, 2026 katika viwanja vya michezo vya Halmashauri pamoja na Nsekela Stadium, ni la kwanza kwa ukubwa wake kufanyika mkoani Kagera likihusisha Halmashauri sita kwa pamoja.
Halmashauri zilizoshiriki ni Kyerwa (mwenyeji), Karagwe, Missenyi, Bukoba Manispaa, Bukoba Vijijini na Muleba.
Washiriki walishindana katika michezo ya Mpira wa Miguu, Mpira wa Pete (Netball), Mpira wa Wavu (Volleyball) na Vishale (Darts).
Katika ushindani huo wa kirafiki na wenye mshikamano, Halmashauri ya Muleba ilitwaa ubingwa wa jumla wa bonanza hilo, huku Kyerwa ikiibuka mshindi wa pili kwa jumla ya michezo yote.
Akifungua rasmi bonanza hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Mhe. Zaituni Msofe, alizitaka timu zote kuzingatia misingi ya fair play, akisisitiza kuwa michezo ni chachu ya furaha, huimarisha mahusiano na kujenga undugu miongoni mwa watumishi.
Aidha, aliwahimiza washiriki kutumia fursa hiyo kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Wilayani Kyerwa ikiwemo hifadhi ya Ibanda-Kyerwa, hifadhi ya Rumanyika-Karagwe pamoja na Majimoto ya Mutagata.
Kwa upande wake, Afisa Michezo wa Wilaya ya Kyerwa, Daima Nkinda, alisema lengo la bonanza hilo ni kuimarisha undugu, urafiki, kufahamiana na kubadilishana uzoefu wa kikazi miongoni mwa watumishi wa serikali.
Bonanza hilo limeacha alama ya mshikamano na kuweka msingi wa kuendeleza mashindano ya aina hiyo katika miaka ijayo, likiwa jukwaa muhimu la kukuza vipaji na kuimarisha afya kwa watumishi wa umma.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment