Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mheshimiwa
John Kahyoza, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Sheria Nchini leo
Februari 02, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga.
Na Mapuli Kitina Misalaba
Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imeadhimisha Siku ya Sheria Nchini leo Februari
02, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga, huku Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mheshimiwa John Kahyoza, akisisitiza kuwa
Mahakama ina nafasi kubwa katika ustawi wa jamii na maendeleo ya Taifa kwa
kutoa haki kwa wakati, kwa wote na bila upendeleo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyoambatana na
kauli mbiu isemayo “MCHANGO WA MAHAKAMA KATIKA USTAWI NA MAENDELEO YA TAIFA”,
Mheshimiwa Kahyoza amesema Siku ya Sheria ni fursa muhimu kwa Mahakama, wadau
wa sekta ya sheria na wananchi kutafakari nafasi ya sheria katika kudumisha
amani, utulivu, umoja na maendeleo ya nchi.
Amebainisha kuwa utamaduni wa kuadhimisha Siku ya
Sheria ulianza rasmi mwaka 1996, ambapo baadaye mwaka 2015 ukaanza mfumo wa
Wiki ya Sheria kabla ya kilele cha Siku ya Sheria na kwamba kwa mwaka 2026,
maadhimisho yamefanyika kwa siku moja kufuatia maelekezo ya ngazi ya Kitaifa,
huku elimu ya sheria ikiendelea kutolewa kwa wananchi kila siku ndani ya viunga
vya Mahakama.
Mheshimiwa Kahyoza ameeleza kuwa tathmini ya utendaji
wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga kwa mwaka 2025 inajumuisha pia Mkoa wa
Simiyu, kufuatia kutangazwa rasmi kwa Mahakama Kuu Kanda ya Simiyu tarehe 19
Desemba 2025.
Kwa mujibu wa takwimu zilizowasilishwa, Mahakama Kanda
ya Shinyanga imeonyesha ufanisi mkubwa katika usikilizaji wa mashauri, ambapo
mashauri 9,490 yamesajiliwa mwaka 2025, mashauri 9,877 yamesikilizwa na kumalizika,
huku mashauri 593 yakibaki hadi Desemba 2025, ikilinganishwa na mashauri 985
yaliyobaki mwaka 2024.
Amesema hali hiyo inaonesha Mahakama inasikiliza
mashauri mengi zaidi kuliko yanavyosajiliwa, hatua inayochangia kupunguza
mlundikano wa kesi na kuongeza imani ya wananchi kwa mhimili wa Mahakama.
Aidha, amefafanua kuwa kwa sasa Mahakama ina shauri
moja pekee la mwaka 2023 lenye kizuizi cha kisheria, huku mashauri mengine
yaliyobaki yakiwa ya umri mdogo, mengi yakiwa ya mwaka 2025. Mkakati uliopo ni
kuhakikisha ifikapo Juni 2026, mashauri yote ya mwaka 2025 yanakuwa
yamesikilizwa isipokuwa pale zitakapokuwepo sababu za msingi.
Mheshimiwa Kahyoza ametaja matumizi ya Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kama chachu ya maboresho ya utoaji wa haki,
akieleza kuwa mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mashauri (eCMS)
umeunganishwa na wadau 13 wa sekta ya haki, hatua inayorahisisha kubadilishana
taarifa, kupunguza ucheleweshaji wa mashauri na gharama kwa wananchi.
Amesema Mahakama imeendelea kuruhusu usikilizaji wa
mashauri kwa njia ya mtandao (video conference), hali inayowawezesha mashahidi
na wadau kufuatilia kesi bila kusafiri umbali mrefu, hivyo kuwapa wananchi muda
wa kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali.
Katika kuwasogezea wananchi huduma za haki karibu,
Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga imeeleza kuwa imefanikiwa kujenga Mahakama za
Mwanzo mpya zenye vifaa vya kisasa Kahama Mjini na Shinyanga Mjini (Majengo –
Nguzo Nane), huku Kanda ikiwa na jumla ya Mahakama za Mwanzo 35.
Pia, huduma za Mahakama Kuu zimesogezwa karibu na
wananchi kupitia kuanzishwa kwa Masjala Ndogo ya Simiyu, huku ujenzi wa masjala
nyingine ukiendelea katika mikoa mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Kahyoza amesisitiza kuwa Mahakama ni
mhimili muhimu katika kulinda Katiba na utawala wa sheria, kulinda haki za
binadamu, kuimarisha uwekezaji, kutatua migogoro kwa amani na kuchangia Dira ya
Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema Mahakama inapotoa haki kwa wakati, imechangia
kufungua shughuli za kiuchumi zilizokwama, kama ilivyodhihirika katika mpango
wa kitaifa wa kusikiliza mashauri ya kimkakati zaidi ya 2,000 yanayohusisha
biashara, ardhi, kodi na uwekezaji, ambapo sehemu kubwa ya mashauri hayo
yamekamilika na kuruhusu mitaji kurejea kwenye mzunguko wa uchumi.
Kwa Kanda ya Shinyanga pekee, jumla ya mashauri 92 ya
kimkakati yametambuliwa, huku baadhi yake tayari yakishapatiwa maamuzi.
Katika hitimisho lake, Mheshimiwa Kahyoza ametoa wito
kwa wadau wote wa sekta ya haki kushirikiana na Mahakama ili kuhakikisha haki
inatolewa kwa weledi, bila ucheleweshaji na kwa kuzingatia maadili. Anawahimiza
Majaji, Mahakimu na Watumishi wa Mahakama kuendelea kuzingatia viapo vyao,
kutoa huduma kwa uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Katika maadhimisho hayo, Wakili wa Serikali Mfawidhi
Mkoa wa Shinyanga, Lameck Merumbe, amezungumza kuhusu umuhimu wa ushirikiano
kati ya Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na taasisi nyingine za
haki katika kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati na kwa maslahi mapana ya
wananchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Kujitegemea Tanganyika (TLS) Mkoa wa Shinyanga, Shaban Mvungi, amezungumzia masuala mbalimbali yanayowahusu wanasheria, ikiwemo maadili ya taaluma, matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma za kisheria na wajibu wa mawakili kushirikiana na Mahakama katika kulinda haki na ustawi wa jamii.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mheshimiwa
John Kahyoza, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Sheria Nchini leo
Februari 02, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga.
Wakili wa Serikali Mfawidhi Mkoa wa Shinyanga, Lameck
Merumbe, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Sheria Nchini leo Februari
02, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Kujitegemea Tanganyika (TLS) Mkoa wa Shinyanga, Shaban Mvungi, akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Sheria Nchini leo Februari 02, 2026 katika viwanja vya Mahakama Kuu Shinyanga.
MC MAMA SABUNI

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254










































Post a Comment