Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. John Mongella akiwa kwenye mradi wa ujenzi wa soko kuu manispaa ya shinyanga mradi unaojengwa kupitia fedha za ndani za halmashauri mradi unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.8.
Na. Elias Gamaya, Misalaba Media - Shinyanga.
Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. John Mongella, ameipongeza halmashauri ya manispaa ya shinyanga kwa ubunifu wa kutekeleza mradi wa Soko kuu lenye jumla ya vyumba 106 kwa lengo la kuboresha mazingira ya wafanyabiashara mradi unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni 1.8.
Ndg. Mongella ametoa pongezi hizi leo Februari 02, 2026, wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi katika kuelekea maadhimisho ya miaka 49 tangu kuanzishwa kwa chama hicho, ambapo Amesema kuwa kukamilika kwa soko hilo ni jambo la msingi katika kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza kipato cha wafanyabiashara na kukuza mapato ya Halmashauri.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Wakili Julius Mtatiro, amesema Serikali ya Wilaya inatambua umuhimu wa kuboresha mazingira ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati. Amesema tayari amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga kwa lengo la kumshauri kuomba vibali husika pamoja na kutafuta wawekezaji ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa haraka na kuanza kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati.
Awali, akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa vibanda 106 vya biashara, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Ndg. Michael Makotwe, amesema mradi huo umekumbwa na changamoto kadhaa, ikiwemo upatikanaji wa malighafi za ujenzi hususan mawe ya kujazia msingi, ambayo hupatikana umbali mrefu na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa kazi.
Kukamilika kwa ujenzi wa Soko Kuu la Manispaa ya Shinyanga kunatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wafanyabiashara na wananchi wa Manispaa ya Shinyanga kwa ujumla, sambamba na kuimarisha mpangilio mzuri wa shughuli za kibiashara ndani ya Manispaa.
Mwomekano wa jengo la soko kuu Manispaa ya Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Wakili Julius Mtatiro, akizungumza kwenye ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Ndg. John Mongella.

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254







Post a Comment